Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimethibitisha kuachiwa huru na kurudishwa jijini Dar es Salaam viongozi wake, akiwamo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwa ulinzi wa polisi.
Mbali na Mbowe viongozi wengine waliorudishwa Dar es Salaam ni makamu mwenyekiti wa chama hicho (bara), Tundu Lissu aliyefika nyumbani kwake Tegeta asubuhi kwa kusindikizwa askari polisi.
Leo Jumanne Agosti 13,2024 katika akaunti yake ya X zamani Twitter, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ameandika, “viongozi wakuu wa Chadema @freemanmbowetz @TunduALissu @jjmnyika @John_Pambalu wamerejeshwa Dar es salaam na polisi na wamejidhamini wenyewe.
“Kuna taarifa za baadhi ya viongozi wa Bavicha (Baraza la Vijana la Chadema) kuendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mbeya, tutatoa taarifa baadaye,” ameandika Mrema.
Hata hivyo, taarifa zinadai kuwa Lissu na baadhi viongozi wa chama wamenyang’anywa simu na Jeshi la Polisi la Mkoa wa Mbeya.
Viongozi hao ni wachache kati ya kundi la wanachama 520 waliokamatwa na polisi kwa madai ya kukiuka zuio la kutofanyika kwa kongamano la maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani inayosheherekewa Agosti 12 ya kila mwaka.
Jana, Agosti 12, 2024 Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Awadh Haji alitangaza kuachiwa kwa viongozi hao na baadhi ya makada.
Hata hivyo, Kamishna Haji amesema polisi haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka sheria na taratibu za nchi kwa kuiga mataifa mengine.
Kukamatwa kwa viongozi hao kulizua mjadala katika mitandao ya kijamii huku makundi mbalimbali ya haki za binadamu na vyama vya siasa, vikishinikiza Jeshi la Polisi liwaachie huru.
Miongoni mwa vyama hivyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM), kupitia katibu mkuu wake, Dk Emmanuel Nchimbi aliyemuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kuona namna ya kuwaachia viongozi wa Chadema waliokamatwa Mbeya.
“Mtupe nafasi na sisi wanasiasa tuzungumze, sio mambo yote yanatatuliwa kisheria, mengine ni ya kisiasa,” amesema Dk Nchimbi aliyepo katika ziara ya chama hicho, mkoani Geita.