Mcameroon aivuruga Chui BDL | Mwanaspoti

POINTI mbili zilizofungwa Mcameroon, Charly Kasseng wa Srelio katika sekunde nne za mwisho za robo ya nne, ziliipa ushindi timu hiyo wa pointi 48-47 dhidi ya Chui, katika ligi ya kikapu (BDL), kwenye Uwanja wa Donbosco, Upanga.

Kabla ya sekunde hizo, Chui ilikuwa inaongoza kwa pointi 47 dhidi ya 46 za Srelio na pointi hizo mbili zilizofungwa,  ni baada ya kocha wa timu hiyo Miyasi Nyamoko kuomba mapumziko ya kurekebisha makosa ‘time out’.

Baadaye Srelio ilianzisha mpira na kumpasia Kasseng  aliyeingia nao ndani ya duara katika goli la Chui na kufunga na mchezo ukamalizika muda huo.

Robo ya kwanza ilivyoanza, timu zote zilianza kwa kusomana mchezo hali iliyofanya zifungane 8-8.

Robo ya pili Chui ilikuja juu na ikafunga pointi 12-10, na hadi mapumziko Chui ilikuwa mbele kwa pointi 20-18, huku robo ya tatu Srelio ikapata pointi 18-9.

Robo ya nne Chui ilibadilika na kuongoza hadi sekunde nne za mwisho, ndipo Kasseng aliwanyanyua mashabiki kwa kufunga pointi hizo muhimu na ushindi.

Katika mchezo huo Ezra Lucumay aliongoza kwa kufunga pointi 12, akifuatiwa na Kasseng aliyefunga pointi 10, huku kwa upande wa Chui, Isaya Aswile alifunga pointi 16, akifuatiwa na Louis Victor, pointi 8.

Katika mchezo mwingine uwanjani hapo, Savio iliishinda DB Oratory kwa pointi 67-47.

Related Posts