Unguja. Mfumko wa bei kwa kipindi cha miezi 12 hadi kifikia Julai 2024 umepungua na kufikia asilimia 5.26 kutoka asilimia 5.65 iliyorekodiwa kwa kipindi cha Juni mwaka jana, Zanzibar.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Agosti 13, 2024 mtakwimu kutoka divisheni ya takwimu na bei, Hassan Jamal Hassan amesema kundi la bidhaa za chakula na vinywaji visivyo na kileo kwa Julai 2024 imepungua na kufikia asilimia 8.96 ikilinganishwa na asilimia 10.33 iliyorekodiwa Juni 2024.
Amesema kwa jumla farisi za bei zimeongezeka na kufikia 112.31 kwa Julai 2024 ikilinganishwa na 106.70 ambayo imerekodiwa Julai mwaka jana 2023.
“Mfumko wa bei wa bidhaa za chakula kwa mwaka unaoishia Julai 2024 umepungua na kufikia asilimia 9.16 ikilinganishwa na asimilia 10.57 iliyorekodiwa Juni 2024. Farisi za bei za bidhaa za chakula kwa Julai 2024 zimeongezeka na kufikia 122.08 kutoka 111.84 iliyorekodiwa Julai 2023 mwaka jana,” amesema.
Amesema bidhaa zisizo za chakula kwa mwaka umeongezeka na kufikia asilimia 2.37 kwa Julai 2024 ikilinganishwa na asilimia 2.07 iliyorekodiwa Juni 2024 mwaka huu.
Amesema bidhaa zisizo za chakula zimeongezeka na kufikia 105.65 kwa Julai 2024 ikilinganishwa na 103.20 iliyorikodiwa Julai 2023 mwaka jana.
Ametaja bidhaa zilizofanya kupungua kwa mfumko huo kwa mwaka ni mchele wa Mbeya asilimia 4.4, unga wa ngano asilimia 4.5, unga wa sembe asilimia 8.8, ndizi za mkono mmoja asilimia 7.5 na ndizi za mtwike asilimia 18.6.
Mfumko wa bei kwa Julai 2024 umepungua na kufikia asilimia 0.22 ikilinganishwa na asilimia 0.56 iliyorekidiwa Juni 2024, huku bidhaa za chakula na vinywaji visio na vilevi umepungua na kufikia asilimia 0.15 ikilinganishwa na asilimia 0.70 iliyorikodiwa Juni.
Mchele wa Mbeya umefikia asilimia 2.0, mchele wa Jasmini asilimia 0.4, samaki asilimia 1.6, ndizi ya mkoni mmoja asilimia 5.2, sukari nyekundu ilikuwa asilimia 1.1 na mafuta ya petroli asilimia 1.5 kwa kwa mwezi uliomalizika.
Meneja Msaidizi Uchumi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) upande wa Zanzibar, Shamy Hamcha amesema hali ya mfumko wa bei kwa Zanzibar inaonekana kwenda vizuri na hali ya kuridhisha.
Amesema kama kisiwa kuna mahitaji lazima kuagizwa kutoka nje, hivyo wananchi wasipate wasiwasi juu ya jambo hilo kwani inaonekana kila mwezi mfumko huo unatoa matumaini na kuwalinda walaji wa bidhaa mbalimbali.
Amesema Benki Kuu imejipanga kuhakikisha hali ya uchumi inakuwa rafiki kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla licha ya kuwa kipindi cha nyuma kidogo hali ya upatikanaji wa Dola ya Marekani ilikuwa ina changamoto lakini kwa sasa hali imerejea katika hali ya kawaida.