Mikakati yaandaliwa, tumbaku ikishika namba mbili mauzo ya bidhaa asili nje

Dar es Salaam. Tumbaku ikishika nafasi ya pili katika mauzo ya bidhaa za asili nje ya nchi mwaka 2023, wadau wanashauri itafutwe njia mbadala ya kukausha zao hilo hasa kwa wakulima wadogo ili kuepusha ukataji miti unaoweza kuligharimu Taifa.

Hata hivyo, Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) katika mazungumzo na Mwananchi imesema tayari kuna aina mbili za mbegu zinazotumia hewa na jua kukauka zimeanza kutumiwa na wakulima katika baadhi ya mikoa.

Ripoti ya Takwimu za Msingi Tanzania 2023 inaeleza kuongezeka uzalishaji wa tumbaku nchini ni moja ya sababu ya mauzo ya nje ya nchi kukua zaidi ya mara mbili,  kati ya mwaka 2021 hadi 2023.

Inaelezwa katika ripoti hiyo kuwa, kukua kwa mauzo kutoka Sh291.4 bilioni mwaka 2021 hadi Sh824.9 bilioni mwaka 2023 kunaifanya tumbaku kushika nafasi ya pili katika mauzo ya bidhaa za asili nje ya nchi na kuleta mapato mengi nchini, ikiipiku korosho ambayo mwaka 2023 ilishika nafasi hiyo.

Ripoti hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inafafanua kuwa siyo mauzo tu ya zao hilo yaliyoongezeka, bali hata bidhaa zinazotokana na tumbaku nazo uzalishaji wake umeongezeka.

Uchambuzi unaonyesha uzalishaji sigara uliongezeka kutoka sigara bilioni 7.02 mwaka 2021 hadi bilioni 11.86 mwaka 2023.

Ongezeko la uzalishaji sigara unaifanya kuwa bidhaa ya pili miongoni mwa baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa viwandani zilizoainishwa na ripoti upande wa Tanzania Bara kati ya mwaka 2019 hadi 2023 ikitanguliwa na bidhaa za  rangi.

Agosti 8, 2024 Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alimweleza Rais Samia Suluhu Hassan kuwa, kama si mvua za El-Nino, Tanzania ingekuwa mzalishaji mkubwa wa tumbaku duniani kwa kuwa hivi sasa inashika nafasi ya pili ikitanguliwa na Zimbabwe.

“…Umechukua uongozi wa nchi yetu uzalishaji wa tumbaku ukiwa ni tani elfu 65 na malengo yetu kwa sasa ilikuwa ni kuzalisha tani 170,000 hadi tani 200,000 lakini tumefikisha tani 122,000,” alisema Bashe.

Mtaalamu wa Uchumi na Biashara kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora amesema Taifa linapaswa kuangalia namna linavyoweza kutumia zaidi fursa ya uzalishaji na uuzaji tumbaku nje ya nchi ili kujiingizia fedha za kigeni.

Amesema fursa hiyo inaweza kutumika zaidi hasa katika kipindi hiki ambacho baadhi ya nchi duniani zinapunguza uzalishaji kutokana na kampeni zinazofanywa kupiga marufuku matumizi ya sigara katika maeneo yao.

“Sisi tunaweza kuimarisha uzalishaji kwa kufanya utafiti kuangalia sehemu ambazo watu wanaweza kulima zaidi tumbaku na kufanya uzalishaji ili kutumia fursa iliyopo,” amesema.

Kuhusu uzalishaji wa sigara kuongezeka, Profesa Kamuzora amesema athari zake kwa watumiaji ni bayana na huainishwa hata kwenye pakiti, akisema kisanyansi kitu chochote kinapotumiwa kupita kiwango kinaweza kumuathiri mtu.

“Kama mtu unakunywa supu ya nyama yenye mafuta mengi kila siku utaishia kupata tatizo, kila kitu unapotumia kwa wingi kina madhara,” amesema Profesa Kamuzora.

Hata hivyo amesema ni vyema kuangalia kama nikotini inaweza kuwaathiri hadi wakulima, kwa kufanya tafiti katika moja ya mkoa unaozalisha kwa wingi tumbaku na kulinganisha na ule ambao hauzalishi.

Amesema moja ya kitu kinachoweza kuangaliwa ni umri wa mtu kuishi.

Ukataji miti kwa ajili ya kupata kuni za kukaushia tumbaku ni suala linalojadiliwa hapa na pale, kwamba kadri uzalishaji unavyoongezeka ndivyo nchi inakuwa kwenye hatari ya kuwa jangwa.

Profesa Kamuzora amependekeza kuwapo mipango ya njia zinazoweza kutumika kukausha zao hilo bila kutumia kuni zinazosababisha ukataji miti.

 “Kuna baadhi ya kampuni niliona zinaotesha miti kwa ajili ya kufidia uharibifu nafikiri tunahitaji kujipanga zaidi kwa kuangalia wapi tunaweza kurekebisha, ikiwemo kupanda miti kwa wingi,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB), Stanley Mnosya amesema njia pekee ya kuzuia ulimaji tumbaku kuathiri mazingira ni kuangalia namna ya kudhibiti ukataji miti.

Amesema kwa sasa wamebadili majiko ya kukaushia tumbaku kwa kuondoa yenye uwezo wa kuingiza magogo na kuweka yanayotumia matawi matawi ya miti pekee.

Amesema wameingia mkataba wa miaka mitatu na moja ya kampuni itakayokuwa ikiwajengea wakulima majiko.

“Lakini ukiacha hili, tuna mbegu mpya aina mbili za tumbaku ambazo zitakuwa hazihitaji moto kukaushia, badala yake zitatumia hewa na mwanga wa jua,” amesema Mnosya.

Amesema mbegu inayokaushwa kwa kutumia hewa huhitaji kivuli, hivyo mkulima atafunika  na nyavu na kuacha sehemu ya kupitisha hewa.

Pia kama mtu ana  miti ya kivuli ana uwezo wa kuweka tumbaku chini yake na ikakauka vizuri.

“Mbegu hizi tayari zimeanza kutumika katika maeneo ya Iringa, Singida na baadhi ya sehemu ya Tabora, lengo letu ni kuona mwaka huu asilimia 30 ya tumbaku yote itokane na mbegu hizi na tutakuwa tukiongeza kidogokidogo hadi zao hili nchi nzima litakapokuwa linatokana na mbegu hizi,” amesema.

Kutokana na baadhi ya tumbaku kuendelea kukaushwa kwa moto amesema kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Misitu unaotegemea Jamii (CBFM) wanalinda watu kutoingia kiholela kukata misitu, bali kwa kufuata utaratibu ambao unaenda sambamba na watu kufundishwa namna ya kuvuna misitu.

Amesema kuna kampeni maalumu inayowataka wakulima kupanda miti 500 anapolima hekta moja, huku vikundi vya kinamama na vijana vimeundwa kusimamia na kutunza miti inayopandwa.

Wakati hayo yakifanyika, bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2024/2025 inataja mkakati katika zao hilo ni kuratibu upatikanaji wa tani 127,316 za mbolea na kusambaza kwa wakulima kwa mpango wa ruzuku.

Hilo litaenda sambamba na usambazaji wa viuatilifu lita 236,329 na pakiti 1,664,286, vifungashio belo 11,709 na nyuzi 166,429 kwa ajili ya kuimarisha uzalishaji wa tumbaku.

Mbolea ya NPK (10:18:24) itaagizwa na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) na kusambazwa kwa wakulima wa tumbaku.

“Bodi ya Tumbaku Tanzania itajenga mabani ya kisasa 2,353 katika mikoa ya Tabora, Shinyanga, Geita, Kigoma, Ruvuma, Katavi, Mbeya, Songwe, Iringa, Morogoro na Mara. Mabani hayo yatasaidia kupunguza upotevu wa majani, kuongeza ubora wa tumbaku na kutunza mazingira,” imeeleza wizara katika bajeti hiyo.

Related Posts