Mwalimu augua, kesi yashindwa kusikilizwa

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeshindwa kuendelea na usikilizwaji wa kesi ya kulawiti mtoto mwenye ulemavu inayomkabili, mwalimu wa mafunzo kwa vitendo, Frank Mpogoma.

Kesi hiyo imeshindwa kuendelea kutokana na mshtakiwa kuugua wakati alipofikishwa mahakamani kwa ajili ya kuanza kujitetea.

Mpogoma ambaye ni mwalimu wa mafunzo kwa vitendo kutoka Shule ya Msingi Maweni iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam anadaiwa kumlawiti mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13, Februari 22, 2023 shuleni hapo.

Kesi hiyo ilipangwa leo Jumanne, Agost 13, 2024 kwa ajili ya mshtakiwa kuanza kujitetea baada ya kukutwa na kesi ya kujibu.

Mpogoma alikutwa na kesi ya kujibu baada ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo anayesikiliza shauri hilo kupitia ushahidi wa mashahidi sita na vielelezo.

Kabla ya kuahirishwa kwa shauri hilo, wakili wa Serikali Asiat Mzamiru alieleza Mahakama hiyo kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya mshtakiwa kuanza kujitetea na upande wa mashtaka upo tayari.

Mzamiru baada ya kutoa maelezo hayo, mshtakiwa alisimama na kudai kuwa anaumwa na hataweza leo kutoa utetezi wake, hivyo aliomba Mahakama ipange tarehe nyingine.

Kutokana na hali hiyo, hakimu Swallo aliahirisha kesi hadi Agosti 26, 2024 itakapoendelea na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Mpogoma alikutwa na kesi ya kujibu baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao wa mashahidi sita na vielelezo viwili.

Miongoni mwa mashahidi wa upande wa mashtaka waliotoa ushahidi wao dhidi ya mwalimu huyo ni Koplo Salome Kiula, kutoka Dawati la Jinsia na Watoto katika Kituo cha Polisi Kigamboni.

Katika ushahidi wake koplo Kiula, alidai mwalimu huyo wa mafunzo kwa vitendo alimlawiti mtoto huyo darasani baada ya kumziba mdomo.

Akiongozwa kutoa ushahidi na wakili Mzamiru, shahidi huyo alidai yeye ni askari mpelelezi na anahusika na dawati la jinsia kituoni hapo, Februari 22, 2023 akiwa kwenye majukumu yake ya kazi walifika wanawake wawili wakiwa na mtoto ambaye ni mlemavu wa miguu.

“Mmoja wa wanawake hao alijitambulisha kama mwalimu Fatuma na mwingine ni mama mzazi wa mtoto huyo. Mwalimu Fatuma alinieleza kuwa majira ya saa moja asubuhi, akiwa Shule ya Msingi Maweni, alisikia mtoto analia darasani,” amedai Kiula na kuongeza.

“Baada ya kusikia kilio mwalimu huyo alikwenda darasani hapo na alikuta mtoto akilia na baada ya kumuhoji, mtoto alimweleza kuwa amelawitiwa na mshtakiwa ambaye alikuwa ni mwalimu wa mafunzo kwa vitendo shuleni hapo,” alidai.

Alieleza siku hiyo ya tukio, mtoto huyo alipelekwa shule na mama yake na kumshusha katika moja ya korido na kuingia darasani.

“Baadaye Mpogoma aliingia akiwa ameshika simu kubwa na kumuonesha muathirika picha za ngono na kumtaka wafanye kama inavyoonesha katika picha hizo,” amedai shahidi.

Shahidi aliendelea kudai muathirika alikataa ndipo Mpogomo alimziba mdomo na kumvua nguo ya ndani, naye akajivu ya kwake na kumlawiti.

Alidai kuwa, mwalimu Fatuma baada ya kutoa maelezo hayo katika dawati hilo la jinsia na watoto, aliwapa fomu namba tatu ya Polisi (PF3), waende hospitali kuthibitisha maelezo hayo.

“Tuliongozana hadi Kituo cha Afya Kigamboni, muathirika alifanyiwa vipimo na kuthibitika kwamba kweli alilawitiwa, tulipewa ripoti ya kitabibu na kurejea kituo cha polisi na mshitakiwa alikamatwa,” amedai shahidi.

Baada ya hapo, koplo Kiula aliandaa jalada la uchunguzi na aliteuliwa kuwa mpelelezi wa kesi hiyo, pia aliandika maelezo ya mashahidi wote muhimu na aliandaa vielelezo.

Shahidi alidai kuwa, walifanya gwaride la utambuzi na mtoto huyo aliweza kumtambua mshtakiwa aliyemfanyia kitendo hicho.

Related Posts