SAKATA la wawakilishi wa Zanzibar kwenye michuano ya kimataifa kuamua kuchezea mechi zao zote ugenini limeibua sintofahamu kwa wadau. Huku wakihoji ; “Nini kiko nyuma ya timu hizo?”
JKU itacheza dhidi ya Pyramids ya Misri mechi zote mbili ugenini sawa na Uhamiaji ambayo pia mechi zake za Shirikisho dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya zitapigwa ugenini,Agosti 18 na 24.
Tayari klabu zote zimeshatoa matamko rasmi, ingawa habari za ndani ni kwamba kuna kampuni za Libya na Misri zenye chembechembe za mashabiki wa timu mwenyeji zilizowaandalia mechi za kirafiki na sehemu za kuweka kambi pamoja na kubeba sehemu kubwa ya gharama za timu hizo, jambo ambalo limewashtua wadau.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Hussein Ahmada, alikiri kwamba Uwanja wa Amaan unafaa kutumika kwa mechi za Caf na klabu husika zinajua hilo.
“Kama inavyofahamika hizi ni timu za Ligi Kuu Zanzibar, huwa na maamuzi yao, sisi kama ZFF kwa nafasi yetu tumefanya kile ambacho kinatakiwa kufanywa katika utaratibu uliokuwa bora zaidi.”
“Klabu hizi za JKU na Uhamiaji zenyewe katika maamuzi yao kama klabu bila shaka wamefikia uamuzi na wapinzani wao kukubaliana sababu kubwa ikiwa ni gharama za maandalizi.
“Sisi kama ZFF tumefanya mawasiliano na CAF kuulizia jambo kama hili linawezekanaje lakini upande wao hakukuwa na shida, kikubwa timu zote mbili zimekubali kushea gharama za mchezo huu.
“Ni kweli mwanzoni Uwanja wa New Amaan Complex haukuwa kati ya viwanja vilivyopitishwa na CAF katika mashindano ya klabu lakini baadaye ukapitishwa lakini klabu zikaamua kwenda kucheza mechi zao zote nje kwa makubaliano maalum,” alisema kiongozi huyo.
Nyota wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa ameshangazwa; “Sijajua kwanini wameamua kufanya maamuzi hayo, nilidhani pengine mechi zao za nyumbani ingekuwa karata muhimu kwao,sote tunajua umuhimu wa kucheza nyumbani huwa na faida ya ziada kutokana na sapoti kutoka kwa mashabiki.”
Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka la Tanzania(TFF), Angetile Osiah alisema kuwa; “Hizi ni taarifa za kushangaza. Kwamba timu mbili zinazomilikiwa na taasisi za serikali zimeamua kuuza uhuru wake na kwenda kuchezea mechi zote mbili kila mmoja ugenini? Kuna viashiria vya kupanga matokeo.”
“Kiongozi wa JKU alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa wapinzani wao wa Libya watawasaidia mambo mengi. Huu msaada unakujaje wakati wa mashindano kama si mipango? Tungeelewa kama kulishakuwa na urafiki awali, au kusingekuwa na uwanja ulioidhinishwa na CAF.”
“Lakini Serikali imetoka kukarabati uwanja wa Amaan ili utumike kwa mechi zote na wananchi wapate burudani, halafu timu zake zinaukimbia uwanja? Hii si taswira nzuri kwa serikali, Zanzibar na taifa zima la Tanzania. SMZ ichukue hatua za haraka kuzuia aibu hii ya kutoweza kuzitunza vyema timu zake kwa safari, malazi, vifaa na miundombinu ya michezo.
“Kibaya zaidi ni sintofahamu inatokea tena kwa timu za taasisi za serikali. Na kingine ni kuwanyima Wazanzibari haki ya kuziona timu zao zikishiriki mashindano ya kimataifa, hata kama hawana uhakika wa kufika mbali.”
Kwa upande wake, Sekilojo Chambua ambaye aliwahi kuwika akiwa na Yanga, alisema; “Ni sawa kuamua kucheza mechi zote ugenini ikiwa nchini mwako labda kuna machafuko au hakuna kiwanja chenye vigezo vya CAF, sasa hatujui kwanini wenzetu wameamua kucheza mechi zote ugenini.”