Wakili wa mlalamikaji katika kesi hiyo, Anwarul Islam, amesema kuwa mahakama kuu mjini Dhakar imeagiza uchunguzi kufanyika kubainisha jukumu la Hasina katika mauaji ya Saeed.
Soma pia:Maandamano ya wanafunzi Bangladesh yawalazimisha Jaji Mkuu na Gavana wa Benki Kuu kujiuzulu
Kesi hiyo iliyowasilishwa na Amir Hamza ilikubaliwa na mahakama hiyo baada ya kusikilizwa. Islam ameongeza kuwa Jaji Rajesh Chowdhury aliamuru polisi kuchunguza kesi hiyo.
Hasina akabiliwa na kesi ya kwanza dhidi yake
Kesi hiyo ni ya kwanza kufunguliwa dhidi ya Hasina kufuatia maandamano makali yaliosababisha vifo vya takriban watu 300, wengi wao wakiwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Washtakiwa wengine kwenye kesi inayomkabili Hasina
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Obaidul Quader, katibu mkuu wa chama cha Awami League cha Hasina, waziri wa zamani wa mambo ya ndani Asaduzzaman Khan Kamal na maafisa wengine wakuu wa polisi.
Soma pia:Bangladesh kuunda serikali mpya ya mpito
Hamza anadai Saeed aliuawa mnamo Julai 19 katika saa za alasiri alipopigwa risasi akivuka barabara wakati polisi wakiwafyatulia risasi wanafunzi na watu wengine waliokuwa wakiandamana dhidi ya upendeleo wa ajira serikalini katika eneo la Mohammadpur mjini Dhaka.
Mlalamikaji alimlaumu Hasina, ambaye anasema alitoa agizo la matumizi ya nguvu kutuliza ghasia hizo. Hamza amesema hakuwa na uhusiano wowote na Saeed lakini aliwasilisha kesi hiyo mahakamani kwa kujitolea kwa sababu familia ya Saeed haikuwa na fedha za kufungua kesi hiyo.
Hamza aapa kuendelea na kesi dhidi ya Hasina hadi mwisho wake
Hamza ameliambia shirika la habari la Reuters kwama yeye ni raia wa kawaida wa kwanza kuonesha ujasiri wa kuchukuwa hatua hiyo ya kisheria dhidi ya Hasina kwa makosa yake na kwamba atasimamia kesi hiyo hadi mwisho wake.
Hasina, ambaye alikuwa waziri mkuu kwa miaka 15 iliyopita, hakuweza kufikiwa kutoa tamko kuhusu kesi hiyo. Washtakiwa wengine Quader na Kamal pia hawakuweza kufikiwa kwa njia ya simu.
Miito yatolewa ya kushtakiwa kwa Hasina kwa mauaji ya zaidi ya watu 300
Hatua hiyo inakuja wakati ambapo kuna miitoa kutoka kwa waandamanaji kuwashitaki Hasina na wafuasi wake kwa mauaji ya zaidi ya watu 300 wanaowajumuisha wanafunzi na raia wakati wa wiki za ghasia za tangu Julai 15.
Hasina alikimbilia uhamishoni nchini India mnamo Agosti 5 na tangu hapo amekuwa akiishi mjini New Delhi.
Serikali ya Bangladesh yasema haitakipiga marufuku chama cha Hasina
Katika hatua nyingine, hapo jana, waziri mpya wa ndani wa Bangladesh, Sakhawat Hossain, aliwaambia wanahabari kwamba serikali haina nia ya kukipiga marufuku chama cha Hasina cha Awami League, ambacho anasema kilitekeleza jukumu muhimu katika harakati za uhuru wa Bangladesh.