Takukuru yawatolea macho wanasiasa | Mwananchi

Moshi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, imewaonya wanasiasa mkoani humo walioanza kujipitisha mitaani na kutoa pombe, vyakula na zawadi ndogondogo ili kuwashawishi wananchi kuwachagua wakati wa uchaguzi.

Imewataka wanasiasa hao kuacha mara moja vitendo hivyo, kwa kuwa ni sehemu ya rushwa na vinachangia kupatikana kwa viongozi wasio sahihi.

Rai hiyo imetolewa leo Jumanne Agosti 13, 2024 na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Musa Chaulo wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari mkoani humo, kuhusiana na rushwa katika chaguzi.

Chaulo amesema Takukuru imepokea taarifa za baadhi ya watu wenye nia za kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani, walioanza kutoa pombe na vyakula kwa wananchi ili kuwaaminisha kwamba wao ni watu sahihi jambo ambalo ni kinyume cha taratibu na sheria.

“Takukuru tumeanza kupokea taarifa za wale wanaowania kugombea, ambao wengine wanatumia nafasi hizo kuwapa watu chakula, nyama, pombe hasa mbege na vizawadi vidogo vidogo kama sukari na vinginevyo, ninachosisitiza na kutoa rai kwa wananchi wa Kilimanjaro, tusikubali kudanganywa, vizawadi vidogo tunavyopewa vitatukwamisha na havitatufanya tupate maendeleo kwenye mkoa wetu,” amesema kamanda huyo.

Amesema msimamo wa Takukuru ni wananchi kuepuka kuchukua cha mtu na kuhakikisha wanawachagua viongozi sahihi watakaoleta maendeleo.

Ametumia nafasi hiyo pia kuwaasa waandishi wa habari kuepuka kutumika vibaya katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa masilahi binafsi.

“Ndugu waandishi wa habari, mna nafasi kubwa katika kutoa elimu ya rushwa kwa jamii, lakini niombe waandishi wa habari, msikubali kutumiwa na watu kipindi hiki cha uchaguzi kwa masilahi ya watu binafsi,” amesema.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Kilimanjaro, Bahati Nyakiraria amesema kunapokaribia chaguzi mbalimbali huwa kuna vitendo vingi vya viashiria vya rushwa kwa wanasiasa wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Pia, amewataka waandishi wa habari kufuata maadili na misingi ya uandishi wa habari ikiwamo kufuata kanuni na sheria zilizowekwa ili kuandika habari pasipo kuegemea upande mmoja.

Related Posts