Uchakataji usiofaa unavyoharibu soko la dagaa Mwanza

Mwanza. Baadhi ya wajasiriamali jijini Mwanza wamelalamikia uchakataji holela wa dagaa, wakisema unaharibu soko la kitoweo hicho.

Wamesema uchakataji unaofanywa na baadhi yao, hauzingatii ubora, badala yake umejikita kwenye tamaa ya fedha, jambo linalopunguza imani ya wateja.

Wajasiriamali hao wamesema hayo jana Jumatatu Agosti 12, 2024 wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo (MSMEs) kuhusu viwango, ubora wa bidhaa za chakula na masoko yaliyoandaliwa kupitia Mradi wa Qualitan unaofadhiliwa Umoja wa Ulaya na kutekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (Unido) kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

“Kuna dagaa wanaitwa ‘wauwau’ ambao wameenea katika mikoa yenye ukame na ukosefu wa dagaa kama Tabora, Mbeya, Dodoma na mingine. Wanaandaliwa katika mazingira yasiyo salama,” amesema Agnes Pius mchakataji wa dagaa jijini Mwanza.

Agnes amesema kinachofanywa na baadhi yao, ni kuwakaanga dagaa hao kwa mafuta ya wanyama ambayo hayastahili kutumiwa na wanachanganya na dizeli ili yasiishe haraka.

“Wale nyama nono wanakaangwa wakiwa na majimaji, hivyo wanahifadhi mafuta mengi, kiafya sio vizuri ndiyo maana ukinunua wanawahi kuharibika,” amesema.

Amewasihi wachakataji kufuatilia kanuni na mafunzo yanayotolewa na wadau mbalimbali ili kujua namna ya kuandaa bidhaa hiyo kwa afya njema ya mlaji.

Katibu wa Mtandao wa Wanawake Wavuvi Tanzania, Fatuma Katula amesema baadhi yao wanafanya hivyo kwa lengo la kupata faida, akiishauri Serikali kuingilia kati.

“Baadhi yao ukiongea nao wenyewe wanachojali ni biashara na sio ubora na usalama wa mlaji, kwa hiyo nitoe wito kwa wachakataji wa chakula nchini tutengeneze bidhaa zenye ubora kwa ajili ya afya ya Watanzania,” amesema Katula.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Ofisa Viwango Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Makao Makuu, Mwajuma Dukulai amesema ni muhimu wajasiriamali kuwa na alama ya bidhaa ili kurahisisha upatikanaji wa soko.

Alama hiyo pia, amesema inatoa hakikisho la bidhaa kwa mtumiaji, kadhalika kumjengea uwezo wa bidhaa yake kuwa katika ushindani wa soko.

 “Wananchi hakikisheni kabla ya kununua bidhaa hizo kwanza angalieni alama ya TBS, pia muangalie mazingira ambayo hiyo bidhaa imeandaliwa,” amesema.

Msajili wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali Manispaa ya Ilemela, Yusuph Okoko amewasisitiza wajasiriamali wadogo na wakubwa kuzalisha bidhaa bora huku akitoa muda wa miezi mitatu kujirekebisha.

“Wazalishaji zalisheni bidhaa bora kwa sababu kama watu wanatumia bidhaa isiyo salama itawasababishia magonjwa na Taifa kutumia gharama kubwa kununua dawa na vifaa vingine vya matibabu,” amesema.

Akizungumzia mafunzo hayo, msimamizi wa mafunzo hayo Mkoa wa Mwanza kutoka Unido, Joyceline Ntobi amesema mradi huo unatekelezwa katika mikoa 10 nchini ili kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo wazalishe bidhaa zenye viwango na ubora.

“Kwenye mradi huu tumelenga wakuwafikia wajasiriamali wasiopungua 1,000 kwa awamu ya kwanza tupo katika mikoa ya kanda ya ziwa kwa maana ya Mwanza, Shinyanga na Kagera.

“Pia, tunatekeleza kwa maana ya Kigoma tukilenga kuwafikia wajasiriamali takribani 1,000 kutoka mikoa 10, kwa awamu ya pili tutaenda mikoa ya kusini na Kaskazini,” amesema.

Related Posts