Udhuru wa hakimu wakwamisha kesi ya RC wa zamani Simiyu

Mwanza. Kesi ya kulawiti inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (RC), Dk Yahya Nawanda imeshindwa kuendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza baada ya hakimu anayeisikiliza kupata udhuru.

Kesi hiyo namba 1883/2024, inayosikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Erick Marley imeahirishwa leo Jumanne Agosti 13, 2024 na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, Stella Kiama.

Kwa mujibu wa Kiama, hakimu anayesikiliza shauri hilo (Marley) anasumbuliwa na maradhi na anapata matibabu katika moja ya hospitali jijini Dar es Salaam.

Amesema upande wa jamhuri katika shauri hilo kwa kutambua kuwa hakimu huyo ana udhuru haukuleta mashahidi wake huku mshtakiwa (Dk Nawanda) naye akiwakilishwa na mdhamini wake (jina linahifadhiwa) kwa kile kinachodaiwa hayuko sawa kiafya.

“Kwa sababu hizo nimeahirisha shauri hilo kwa niaba ya Mheshimiwa Marley hadi Septemba 10, saa nne asubuhi litakaposikilizwa kwa siku tatu mfululizo,” amesema Kiama.

Julai 16, 2024 mbele ya hakimu Marley, mashahidi wawili wa jamhuri ambao ni mwanafunzi anayedaiwa kulawitiwa na Dk Nawanda na mama mzazi wa mwanafunzi huyo walifungua ukurasa wa kutoa ushahidi ambapo waliutoa nyuma ya kamera (faragha).

Kesi hiyo iliitwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, Julai 9, 2024, mbele ya Hakimu Marley ambapo mshtakiwa alikana shtaka hilo baada ya kusomewa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Magreth Mwaseba.

Dk Nawanda anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 2, 2024, katika maegesho ya magari yaliyoko eneo la Rock City Mall wilayani Ilemela, Mkoa wa Mwanza kinyume na kifungu namba 154 (1) (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16.

Related Posts