Musoma. Jeshi la Uhamiaji mkoani Mara limewakamata wahamiaji haramu 21 wanaodaiwa kuingia nchini kinyume cha sheria, kati yao wamo watoto wawili raia wa Burundi na Uganda.
Watu hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali mkoani Mara, ikiwamo kwenye kizuizi cha magari kilichopo Kijiji cha Kirumi, wilayani Rorya na kwenye daraja la Mto Mara.
Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Mara, Kagimbo Alphonce akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa leo Jumanne Agosti 13, 2024, amesema wahamiaji hao wamekamatwa baada ya kufanyika operesheni maalumu iliyofanywa na jeshi hilo.
“Kutokana na wimbi kubwa la wahamiaji haramu kutoka Burundi na Uganda kuingia nchini, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji alitoa maelekezo tuongeze nguvu katika mapambano haya. Katika mwezi huu tumefanikiwa kuwakamata watu 21,” amesema ofisa huyo.
Alphonce amesema katika operesheni hiyo, raia 16 kutoka Burundi wamekamatwa, wanaume 11 na wanawake watano.
Aidha amesema raia watano kutoka Uganda pia wamekamatwa na wote ni wanaume.
Amesema wahamiaji haramu wengine wamekamatwa eneo la Makoko katika Manispaa ya Musoma, wakielekea Ziwa Victoria kuelekea Kenya.
Amesema taratibu za kuwafikisha mahakamani zinaendelea.
“Msako utaendelea kuwatafuta wote waliongia nchini kinyume cha sheria. Tunawaonya raia wa kigeni wanaotaka kuingia au kupita nchini kuwa hakuna kipingamizi, lakini wanapaswa kufuata taratibu na wawe na nyaraka zinazotakiwa.”
Mmoja wa wahamiaji hao, Ninyokuru Gerald kutoka Burundi akizungumza na Mwananchi, amesema aliondoka nchini kwake kwa lengo la kutafuta maisha bora nchini Kenya kabla ya kukamatwa mkoani Mara.
“Nilidanganywa kwamba Kenya kuna maisha mazuri, hivyo hapa nilikuwa napita tu kuelekea Kenya kutafuta maisha hayo,” amesema.
Raia wa Uganda, Billy Lwazi amesema aliingia mkoani Mara kwa lengo la kuleta bidhaa za nywele na si vinginevyo.
“Nilikuja kwa biashara, nikienda kuagiza bidhaa. Nitalazimika kufuata taratibu ili kufanya biashara vizuri,” amesema mtu huyo.
Baadhi ya wakazi wa Musoma waliozungumzia operesheni hiyo wamesema inapaswa kuwa endelevu, hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa ili kuepuka watu wasiokuwa na sifa kushiriki uchaguzi huo.
Robert Maingu amesema: “Tuko mpakani na kuna muingiliano mkubwa. Watu wasiokuwa wema wanaweza kutumia nafasi hii kupiga kura au kugombea. Vyombo vya usalama viwe makini sana.”
Naye Anna-Rose Werema amesema Uhamiaji inapaswa kuwa makini hasa katika njia zisizo rasmi zinazotumika kuwaingiza wahamiaji hao haramu nchini, badala ya kushughulika na zilizo rasmi pekee.