Wasafiri Stesheni ya Mpanda walia kupigwa jua, mvua

Katavi. Wasafiri wanaotumia treni wamesema wanakumbana na changamoto ya kukosekana eneo la kupumzikia katika Stesheni ya Mpanda mkoani Katavi, hali inayosababisha wanyeshewe na mvua na kuchomwa na jua.

Wamesema wamekuwa wakikaa juani na kunyeshewa na mvua kutokana na kukosekana kwa eneo la abiria kupumzika.

Mwananchi imefika stesheni hapo leo Jumanne Agosti 13, 2024 kuzungumza na baadhi ya wasafiri waliokuwa wamepanga foleni juani wakisubiri kukata tiketi.

Wengi walionekana kuchoka na nyuso zao zilikuwa zimekunjamana kutokana na jua kali linalowaka.

Hata hivyo, Mkuu Mwandamizi wa Stesheni ya Mpanda, Emmanuel Mtawali amesema suala la kukosekana kwa jengo la kupumzika abiria wakati wa kusubiri treni linafanyiwa kazi.

“Serikali ipo kwenye mpango wa maboresho makubwa ya stesheni hii. Tunaahidi kuwa mazingira yataboreka na abiria watafurahia huduma zetu. Kwa sasa, tunakiri kuwa abiria wanateseka kwa jua na mvua kipindi cha masika,” amesema.

Pia,amekiri kuwapo kwa changamoto ya upatikanaji wa tiketi za kielektroniki hali inayosababisha wasafiri kupanga foleni kwa muda mrefu.

“Ni kweli kumekuwa na ucheleweshaji katika kukata tiketi kutokana na matatizo ya mtandao. Tunafanya jitihada za maboresho ili kumaliza changamoto hii,” amesema mkuu huyo mwandamizi wa stesheni ya Mpanda.

Msafiri, Scholar Juma amesema stesheni hiyo ina changamoto nyingi katika utoaji huduma.

 “Hapa, abiria hawana eneo la kupumzika wakati wanasubiri usafiri. Hali hii inaumiza licha ya kulipa nauli na kodi nyingine. Tunalalamika kuhusu hali hii kwa sababu hakuna jitihada za kuboresha mazingira ya stesheni kila mara ni ahadi tu,” amelalamika msafiri huyo.

Tatizo lingine linalowakera abiria ni upatikanaji wa tiketi, Scholar amesema wanakaa kwenye foleni kwa saa zaidi ya mbili hadi tano bila kupata huduma.

“Nimefika hapa tangu saa moja asubuhi ili nikate tiketi, lakini mpaka sasa saa 6:30 mchana bado nipo kwenye foleni. Sijui kuna shida gani hapo ndani,” amelalamika Juma.

Naye msafiri Boniface Mwalimu, amesema tiketi hazitoki kwa wakati na kuna usumbufu mkubwa wakati wa ukataji wake.

“Watu wanachukua vitu kidogo kwa wahudumu ili kupata huduma. Tunaomba Serikali ituangalie na kuboresha mazingira ya stesheni hii,” amesema Mwalimu.

Related Posts