Dar es Salaam. Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Kongamano la Kisayansi la Kimataifa la Matumizi ya Mawimbi Sauti katika Tiba (ISMRM) pamoja na Tiba ya Mishipa ya Fahamu (Neuroradiology) litakalofanyika Septemba 19 hadi 20, 2024 jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo limeratibiwa nchini na Chama cha Madaktari Bingwa wa Rediolojia Tanzania (Taraso); Chama cha Wataalamu wa Rediolojia Tanzania (TARA); Chama cha Wahandisi na Wateknolojia wa Vifaa Tiba Tanzania (AMETT), Shirikisho la Fizikia la Tiba Afrika (FAMPO) kwa pamoja na Wizara ya Afya kupitia Darasa la Wataalamu wa Rediolojia (MRIPC) na Idara ya Huduma za Uchunguzi.
Akizungumza leo Jumanne Agosti 13, 2024 jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya ISMRM na Daktari Bingwa wa Radiolojia kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, Dk Mary Kamuzora amesema kongamano hilo ni la pili kufanyika na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
Dk Kamuzora amesema wataalamu takribani 250 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na Ulaya wanatarajiwa kushiriki kujadili namna ambavyo mapinduzi ya teknolojia yatakwenda kuboresha utolewaji wa huduma za afya.
“Pia, mada pamoja na tafiti mbalimbali zitawasilishwa na wataalamu wa radiolojia kutoka Afrika, Asia, Marekani pamoja na Ulaya,” amesema.
Awali, Dk Kamuzora amesema kongamano hilo litatanguliwa na warsha itakayofundisha wataalamu kuhusu teknolojia mpya ya mashine ya uchunguzi wa magonjwa (MRI) kuanzia Septemba 17 hadi 18, 2024 pamoja na kutoa elimu juu ya faida za kipimo hicho.
Naye Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Radiologia na Mhadhiri Mwandamizi kutoka katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Dk Lulu Fundikira amesema wataalamu hao pia wameandaa onyesho ya mavazi ya utamaduni wa Kiafrika yenye michoro na picha ya kipimo cha MRI linalotarajiwa kufanyika jioni ya Septemba 19, 2024.
“Onyesho hilo limelenga kuonyesha mchanganyiko wa sayansi ya MRI na utamaduni wa Kiafrika lakini pia kutakuwa na harambee kwa ajili ya kufadhili na kuwawezesha watafiti wachanga na wanafunzi ambao wapo katika taaluma hii ya MRI,” amesema.