Karagwe. Mtu mmoja anayedhaniwa kuwa jambazi ameuawa na polisi wa doria akidaiwa kuvamia maduka mawili katika mji mdogo wa Omurushaka, Karagwe, mkoani Kagera.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Agosti 9, 2024, saa saba usiku.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda, amethibitisha tukio hilo leo Jumatano, Agosti 14, 2024.
Amesema watu hao wanaodaiwa kuwa majambazi walivamia maduka ya simu na huduma za kifedha yanayomilikiwa na Godi Basheka na Donatus Kategaya, saa saba usiku wa kuamkia Agosti 9, 2024.
Jeshi la Polisi lilipata taarifa na kufika eneo la tukio, ambapo walikabiliana na watu hao, ambao walijibizana kwa risasi.
Katika majibizano hayo, jambazi mmoja alipigwa risasi mguuni na baadaye kufariki dunia na uchunguzi unaonyesha mtu huyo ni mkazi wa Geita, anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 na 26.
“Jeshi la Polisi linaendelea na ufuatiliaji kubaini mahali walipo wenzake sita waliokimbia baada ya kutekeleza tukio hilo, na baada ya hapo tutatoa taarifa zaidi,” amesema Kamanda Chatanda.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, mlinzi wa maduka hayo, Tauline Theonest, amesema aliwaona watu hao wakiwa na bunduki, mashoka na mapanga na hivyo akajibanza kwenye uchochoro.
“Mara akaja mama mmoja pale nilipokuwa akaniambia watu hao waliopita ni majambazi, tusiendelee na mazungumzo wasije wakatuua,” alisema mlinzi huyo.
Mlinzi mwingine aliyekuwa akilinda kituo cha kuuzia mafuta aliwapigia simu polisi, ambao walifika na kuanza kurushiana risasi, na hatimaye jambazi mmoja alipigwa risasi na kufariki dunia papo hapo.
“Mpaka polisi wanafika, walikuwa wameshavunja na kuiba fedha na vitu vingine,” aliongeza mlinzi huyo.
Mmiliki wa duka la huduma za kifedha, Donatus Kategaya, amesema alikuta maduka yake yamevunjwa na kuibiwa zaidi ya Sh5 milioni. Mmiliki mwingine, Godi Basheka, amesema ameibiwa Sh6 milioni, simu, na vocha.
Hata hivyo, amepongeza Jeshi la Polisi kwa hatua ya haraka iliyochukuliwa na ameomba liimarishe ulinzi katika maeneo yao.
Mwenyekiti wa kijiji cha Omurushaka, Ndibalema Kanyambo, amewashauri wafanyabiashara kuajiri walinzi wenye silaha za moto ili kuimarisha usalama kutokana na hatari ya uvamizi wa majambazi.