Angalizo latolewa kabla ya kufungwa Ziwa Victoria

Mwanza. Siku moja baada Serikali kuitaka Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) kuandaa mkakati wa kulifunga ziwa hilo, wadau wameshauri mambo ya kufanya kabla ya kulifunga.

Ushauri huo umetokana na kauli ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexender Mnyeti aliyoitoa kwenye kongamano la Ukuzaji viumbe Maji jijini Mwanza, akiiagiza Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) kuja na mkakati wa kufunga Ziwa Victoria ili kutoa nafasi ya kupumua na viumbe maji kuzaliana na kuongezeka.

Akizungumza na Mwananchi leo, Jumatano Agosti 14, 2024, Ofisa Mazingira kutoka Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo ya Kiuchumi (Emedo), Lawrence Kitogo amesema ili kutekeleza jambo hilo, watunga sera kutoka nchi zote za Kenya Uganda na Tanzania zinazonufaika na ziwa hilo, wanapaswa  kukutana na kukubaliana siku za kulifunga.

“Kwa kuwa nchi zote ni wanufaika, hivyo lazima wakae chini wakubaliane kuhusu kusudio hilo,” amesema Kitogo.

Mwenyekiti wa kikundi cha Kusimamia Usafi Maeneo ya Fukwe (BMU) Mkuyuni, Robert Charles amesema maisha ya wakazi wa Kanda ya Ziwa chanzo chao cha uchumi ni mazao ya Ziwa Victoria.

Amesema kusitishwa shughuli za uvuvi huenda kukaathiri maisha yao kimapato na hiyo amesema haitakuwa kwa mtu mmoja mmoja, huenda athari hiyo ikaenda mbali zaidi.

“Watu wengi wanategemea uvuvi ukanda huu wa Victoria, tukifunga tutapata athari kubwa ukizingatia shughuli kubwa ya wakazi wake ni uvuvi, niiombe Serikali itafute namna nyingine ila sio hii, kwa sababu itaenda kuathiri mpaka pato la Taifa na hata soko pia,” amesema Charles.

Profesa Yunus Mgaya, Mtafiti na mtaalamu wa Uvuvi na Ufugaji Viumbe Maji wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema; “Samaki wenyewe hawana mipaka, wanaenda kokote kule, kwa hiyo utajikuta watu wako wanaingia katika mtikisiko wa kiuchumi wakati wengine wananufaika.”

Hata hivyo, amesema kulifunga ziwa kwa maana ya uvuvi usiendelee kwa muda sio jambo geni katika uvuvi.

Profesa huyo amesema kuna vitu vitatu vinavyopaswa kuzingatiwa ambavyo ni pamoja na wavuvi, samaki na mazingira walipo samaki.

“Sasa uvuvi ukiendelea kwa kuzingatia usawa wa idadi ya wavuvi watakaoendana na uwingi wa samaki na mazingira yakawa safi, tutakuwa na uvuvi endelevu,” amesema Profesa Mgaya.

Akiunga mkono hoja hiyo, msimamizi wa miradi ya Pwani na Bahari kutoka Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), Dk Modesta Medadi mbali na kuunga mkono hoja ya ziwa kufungwa, ametahadharisha madhara yanayoweza kutokea kwa wavuvi na wananchi kama hawatatafutiwa njia mbadala.

“Kunaweza kusababisha mtikisiko wa kijamii kwa sababu watu wanategemea sana samaki na dagaa kwa chakula, kwa hiyo kwa huku ni ngumu sana kwa sababu pia inahusisha mataifa mbalimbali kama Kenya, Uganda na Tanzania,” amesema Dk Medadi.

Wavuvi, wamiliki wa mitumbwi wafunguka

Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya wavuvi katika Mwalo wa Mswahili uliopo jijini Mwanza wamesema hawakubaliani na suala hilo huku wakipendekeza Serikali ije na mbinu nzuri zaidi ya kukabiliana na upotevu wa samaki na viumbe maji wengine.

“Likifugwa tutaathirika zaidi kwa sababu wengine tuna mikopo kutoka benki na tunarejesha kila wiki kupitia kazi hii ya uvuvi, sasa wakilifunga kwa miezi mitatu hatutarejesha na huenda tukafilisiwa mali tulizoweka dhamana kwenye mabenki,” amesema Benedicto Charles, mvuvi wa mwalo wa Mswahili.

Naye Baraka Masunga amesema baadhi ya wavuvi huendesha maisha yao kwa uvuvi tu, ziwa likifungwa ni sawa na kuwazika wakiwa hai.

“Kuna mtu hajawahi kufanya shughuli za nchi kavu tangu azaliwe maisha yake ni uvuvi tu, sasa mtakapomfungia ataishi vipi, napendekeza tuendelee kufunga hizo siku 10 kila mwezi kama ilivyo sasa,” amesema Masunga.

Mmiliki wa mitumbwi katika Mwalo huo, Alex Maiko ameiomba Serikali iwawezeshe kwanza kiuchumi kwa kuwapatia mikopo ndipo wafanya uamuzi wa kulifunga.

Mchuuzi wa dagaa na samaki katika mwalo huo Angelina Deogratius amesema kwa miaka mingi sasa anaendesha maisha yake kwa kazi hiyo.

Amesema kama ziwa hilo litafungwa, hana biashara nyingine ya kufanya na atakuwa ameweka rehani maisha yake na familia inayomtegemea.

Mchuuzi wa dagaa katika mwalo wa Mswahili, Amina Rashidi ameiomba Serikali kuendelea kufunga shughuli za uvuvi Ziwa Victoria kwa siku 10, badala ya miezi mitatu inayokusudia.

“Hapa tulipo tunalitegemea ziwa kwa kiwango kikubwa kwa sababu tunasomesha watoto na kuendesha maisha yetu kwa ziwa hili, hii ya kulifunga hapana,” amesema Amina.

Related Posts