Balaa Yanga! Siri za Gamondi zabainika, kazi ipo Ligi Kuu

MIONGONI mwa mambo ambayo yamekuwa yakiibeba Yanga ya Miguel Gamondi kimbinu ni pamoja na viungo wake akiwemo Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli kuwa na uwezo wa kucheza baina ya mabeki wa kati na pembeni ‘half-spaces’ kitu ambacho kimekuwa kikiwaweka wapinzani wao katika wakati mgumu.

Katika michezo sita iliyopita kwa Yanga ikiwemo mitatu iliyocheza Afrika Kusini wakati wa maandalizi ya msimu huu kabla ya kurejea Tanzania na kucheza mchezo mmoja katika kilele cha Wiki ya Wananchi na miwili ya Ngao ya Jamii, timu hiyo imefunga mabao 13, asilimia kubwa (8) yamechochewa na uchezaji wa nyota hao.

Kivipi? Wakati Yanga ikifanya mashambulizi yake, mawinga wake huibia mara moja pembeni kisha huacha nafasi kwa mabeki wa pembeni huku wao wakiingia ndani na kuongeza idadi ya viungo kiasi cha wapinzani wao kuwa na wakati mgumu katika namna ya kuwadhibiti, ni wepesi katika kuachia mipira kwa pasi fupifupi wakitafuta nafasi za kupenya kwa kushirikiana na Stephane Aziz KI ambaye amekuwa akicheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho.

Mfano mzuri ni namna ambavyo lilipatikana bao la ushindi kwa vijana hao wa Gamondi katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, zilipigwa pasi 14 kabla ya bao kufungwa, Pacome na Nzengeli kila mmoja aligusa mpira akiwa eneo la kati wakihama pembeni.

Uwezo wa kupasiana kwa haraka huku wakijua nani anatakiwa kuwa wapi na kwa wakati gani uliwafanya kulazimisha wakiwa eneo hilo na kupata nafasi ya bao ambalo lilifungwa Nzengeli na kuifanya Yanga kutinga fainali ambako kwenyewe balaa lao liliendelea kama ilivyokuwa katika dabi.

Licha ya Kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo kuanza na mabeki watatu wa kati, Yannick Bangala, Yeison Fuentes na Yoro Diaby ili kuziba mianya hiyo bado walijikuta kuwa wazi na kufungwa mabao mawili ambayo yalitokea eneo la kati, lile la kusawazisha lililofungwa na Prince Dube na la nne ambalo lilifungwa Clement Mzize.

Mashambulizi hayo, msingi wake ulikuwa eneo la kati, Muadhir Yahya na Clatous Chama walikuwa na mchango mkubwa katika upatikanaji wake, bao la Stephane Aziz KI na alilojifunga Yoro yalitokea pembeni. Yanga ina nguvu kubwa eneo la kati, moja ni kutokana na aina ya wachezaji walionao, pili nguvu ambayo wachezaji wake wa pembani wamekuwa wakiiongeza.

Pamoja na kwamba Gamondi amekuwa akiwatumia mawinga wake kwa kucheza ndani, bado ufanisi wa kujenga mashambulizi kutokea pembeni ni mkubwa kutokana na uwepo wa Chadrack Boka na Yao Kouassi Attohoula.

Tukirejea nyuma hata katika ule mchezo wa fainali ya Kombe la Toyota ambalo Yanga ilialikwa kule Afrika Kusini, unaweza kuona mabao yote ambayo waliyapata wakati wakitoa dozi ya 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs, msingi wake ulikuwa eneo la kati licha ya mabadiliko ya kikosi yaliyokuwa yakifanywa.

Hata yale ambayo mabeki wa Kaizer Chiefs walifanya makosa kama lile lilofungwa na Aziz KI ilikuwa ni matokeo ya presha ambayo wachezaji wa eneo la kati waliitengeneza wakati wakiutafuta mpira.

Miongoni mwa vitu ambavyo vinaonekana kuongezeka kwa Pacome ni namna anakuwa msaada wakati timu ikiwa haina mpira, kwa Nzengeli wala sio tabu kwake amekuwa wa kwanza kuwapa presha wapinzani wao kuanzia juu huku kasi waliyonayo ikiwa msaada jambo ambalo linawanyima uhuru wapinzani wao.

Wakati Yanga ikiwa haina mpira, mawinga hutanua kidogo pembeni ni kutoa sapoti ya kuutafuta mpira kwa mshambuliaji wa mwisho ambaye huwa na jukumu la kwanza kukaba kitu ambacho wamekuwa wakikifanya vizuri Dube na hata Mzize.

Akiliongelea hilo, kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Gwambina, Mohammed Badru amesema ni ngumu kukabiliana na timu inayoanza kukaba kuanzia katika eneo lenu ni rahisi kufanya makosa kama mabeki wakiwa hawana utulivu.

“Nimekuwa nikipenda vile Yanga inaanzia kukabia juu, mpira siku hizi umebadilika hadi ufike katika eneo lao inahitaji kuwa na timu yenye uwezo wa kutegua mitego, kitu kama hicho nimekiona pia kwa Simba, kukabia nyuma ni kumruhusu mpinzani wako akushambulie,” alisema kocha huyo.

Gamondi mbinu zake hizo zimeonekana kutikisa ndani ya siku 14 baada ya kubeba makombe mawili. Julai 28 alianza na Toyota kule Afrika Kusini akiifunga Kaizer Chiefs 4-0, kisha Agosti 11 ilikuwa zamu ya kubeba Ngao ya Jamii kwa kutembeza dozi ya mabao 4-1 mbele ya Azam.

Related Posts