Diwani alalama Sh20 milioni kutojenga zahanati ya kijiji kisa mfumo

Manyara. Diwani wa Naisinyai wilayani Simanjiro, mkoani Manyara, Taiko Laizer ametoa malalamiko mbele ya Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, kuhusu kucheleweshwa kutumika kwa Sh20 milioni za mwekezaji.

Imeelezwa kuwa mwekezaji kutoka Kampuni ya Franone Mining LTD, Onesmo Mbise aliweka kwenye akaunti ya Kijiji cha Naepo wilayani Simanjiro mkoani hapa Sh20 milioni za ujenzi wa zahanati, lakini zimeshindwa kutumika kwa kile kinachodaiwa mfumo kutofanya kazi.

Laizer ametoa malalamiko hayo leo Jumatano Agosti 14, 2024 kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na Ole Sendeka na kufanyika Kata ya Naisinyai.

Amesema mpaka sasa mfumo wa fedha haujasoma taarifa za fedha zilizowekwa, hali inayozuia maendeleo ya mradi huo unaosimamiwa na kijiji.

“Tulitarajia kukamilisha zahanati ya kijiji cha Naepo kwa kutumia Sh20 milioni kutoka kwa mwekezaji, lakini tunakutana na vikwazo vya mfumo usiosoma, hili haliwezekani,” amesema Laizer.

Amesema wananchi wanataka huduma hawawezi kuelewa kama kauli za mfumo kukwama; “Wanachotaka wao ni zahanati yao ijengwe.”

Amesema kama fedha tayari zimeshawekwa kwenye akaunti, maana yake zinapaswa zianze utekelezaji wa kazi kusudiwa na si vinginevyo.

“Watendaji walishughulikie hili haraka, mimi naona wanatuandalia mazingira mabaya kwa wananchi ambao wanatuhoji kutofanya matumizi sahihi ya fedha zilizopo kwenye akaunti, hivyo hili lishughulikiwe ili wananchi wasivunjike moyo,” amesema diwani huyo.

Akijibu malalamiko hayo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amemuhakikishia Laizer kuwa suala hilo linashughulikiwa, akieleza kuwa mfumo wa fedha mara nyingi huwa na changamoto mwanzoni mwa mwaka wa fedha.

Nina imani hali itatengemaa muda si mrefu na tutarudi kwenye matumizi yetu kama kawaida,” amesema mwenyekiti huyo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer, ametoa rai kwa Mbunge Sendeka, Kanunga na Laizer kufuatilia ujenzi wa barabara fupi inayounganisha Emishiye na Lengasiti, ili kupunguza mzunguko mrefu unaosababishwa na mji mdogo wa Mirerani.

Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge Sendeka amesema wamefanikisha ujenzi wa zahanati kwenye kila kijiji cha Kata ya Naisinyai na miradi ya umeme imefika katika vijiji vyote vitano.

“Maji tumefanikisha maeneo yote na sasa tutahakikisha minara ya mawasiliano ya simu inakuwepo na barabara ya Emishie hadi Lengasti na Emishie hadi Landanai inafunguka kuliko kuzungukia Mirerani,” amesema Sendeka.

Related Posts