MSHAMBULIAJI mpya wa Singida Black Stars, Joseph Guede aliyekuwa akikipiga Yanga msimu uliopita amechimba mkwara mpema akisema anatarajia msimu bora kutokana na wachezaji waliopo.
Guede aliyeitumikia Yanga kwa miezi sita baada ya kusajiliwa dirisha dogo kuchukua nafasi ya Hafiz Konkoni ameliambia Mwanaspoti kuwa ameshamalizana na mabingwa wa soka nchini vizuri na ndio waliohusika kwa kiasi kikubwa dili la kutua Singida BS na anaitazama sasa kama timu pinzani.
“Nafurahia maisha ndani ya Singida. Nimekutana na vipaji vingi vikubwa na naamini nitakuwa na msimu mzuri kutokana na kuizoea ligi na kuwa kwenye kikosi cha wachezaji wengi wenye uchu wa mafanikio,” alisema Guede aliyeondojka Yanga akiifungia mabao sita ya Ligi Kuu na matatu ya Kombe la Shirikisho.
“Kuhusu kuizungumzia Yanga na usajili walioufanya sio rahisi kwani sasa ni wapinzani wangu. Napenda kuzungumzia timu niliyopo ambayo nina furaha nayo na natarajia mambo makubwa nikiwa na timu hii ambayo imeniamini.”
Akizungumzia bao la kwanza alilofunga akiwa na timu hiyo kwenye tamasha la Singida Big Day dhidi ya Aigle Noir, alisema limefungua msimu na kazi yake ikiwa ni kufunga anatamani kufanya hivyo kila mchezo.
“Mimi ni mshambuliaji kazi yangu ni kufunga na hakuna mchezaji ambaye anacheza nafasi kama yangu anaingia uwanjani kwa lengo la kuchezea mpira tu bila kufunga nimejiunga na Black Stars kwa lengo la kuhakikisha naipambania inafikia malengo,” alisema mchezaji huyo.
Mbali na mabao tisa ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho, pia mshambuliaji huyo aliifungia Yanga bao moja katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.