Kalambo aichomolea KenGold jioni | Mwanaspoti

ALIYEKUWA kipa wa Dodoma Jiji, Aaron Kalambo ameshindwa kujiunga na KenGold iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya kushindwa kukubaliana maslahi binafsi licha ya kufanya mazoezi kwa takribani wiki tatu.

Nyota huyo wa zamani wa Tanzania Prisons na Geita Gold, aliachana na Dodoma Jiji msimu uliopita, hivyo mabosi wa KenGold wakaanza mazungumzo ili ajiunge na timu hiyo, lakini dili hilo limekwama.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa KenGold, Fikiri Elias ameliambia Mwanaspoti kuwa mchezaji huyo ameondoka kutokanana kushindwa kufikia makubaliano.

“Ni kweli tulikuwa naye na alishaanza mazoezi na wenzake kwa takribani wiki tatu ila alikuwa bado hajasaini mkataba kwa sababu tulikuwa katika mazungumzo, mwishoni akatuambia ofa tuliyomuwekea hajakubaliana nayo hivyo akaondoka,” alisema  Elias aliyewahi kuinoa Coastal Union.

Kalambo alipotafutwa na Mwanaspoti alikiri kuondoka KenGold, akitaja suala la maslahi.

“Kwa sasa siwezi kusema nitacheza wapi kwa sababu bado niko katika mazungumzo na baadhi ya klabu, hivyo nitakapokamilisha kila kitu mashabiki wangu watafahamu nitakapokwenda,” alisema Kalambo, huku Mwanaspoti likiwa na taarifa viongozi wa timu hiyo wako katika mazungumzo na Fountain Gate ili kumpata  Fikirini Bakari aliyejiunga msimu huu akitokea Singida Black Stars.

Related Posts