Kigwangala aibuka na mpya | Mwananchi

Dar es Salaam. Mbunge wa Nzega Vijijini (CCM), Dk Hamis Kigwangalla amesema licha ya Serikali ya Tanzania kuwa na sera na mipango mizuri, kuna tatizo la utekelezaji, hali inayorejesha nyuma utoaji wa huduma za jamii nchini.

Ameyasema hayo leo Jumatano, Agosti 14, 2024 alipokuwa akihutubia katika uzinduzi wa mkakati wa Shirika la Water Aid kwa kuwashirikisha wadau wa maji na usafi wa mazingira (WASH) jijini Dar es Salaam.

Kigwangalla, ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha wabunge wanaopiga vita usugu wa dawa Tanzania, amesema kuna haja ya kuwashirikisha wadau ili kuhakikisha sera na mipango ya Serikali inatekelezwa.

“Tanzania tuna mipango na sera nzuri, lakini tatizo ni kwenye utekelezaji. Kwa mfano, ukitazama sera ya maji, kila kitu kimo mle. Tuna wasomi wazuri ambao wamesoma na wamehitimu vizuri sana, wanaweka mipango vizuri lakini tunakwama kwenye utekelezaji,” amesema.

Amesema kupitia mkutano huo, wadau waazimie kuweka mikakati ya kufanikisha mipango iliyowekwa.

“Kwanza ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa fedha za kutosha kwenye miradi ya maji na usafi wa mazingira kwa ujumla wake, na pili ni kuhakikisha wadau wote wanakuja pamoja kusukuma ajenda hiyo ya mazingira kwa lengo la kumpa kipaumbele mwanamke.

Tatu, tunapaswa kuielimisha jamii ili kila mmoja ashiriki. Kwa mfano, unakuta kampuni kubwa za biashara (anazitaja), wananunua mazao, wanafanya kazi na wananchi. Wananchi wanaweza kujenga vyoo kwenye zahanati, wanaweza kufanya hivyo,” amesema.

Waziri huyo wa zamani wa Maliasili na Utalii amesema kuna haja ya kufanya tathmini na usimamizi kwa kupata taarifa sahihi ili kujua utekelezaji umetoka wapi na utafika wapi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Water Aid Tanzania, Anna Mzinga amesema licha ya dhamira njema ya Serikali, bado upatikanaji wa maji hauridhishi.

“Tumeona kuna vituo vya afya ambavyo huduma za maji na usafi wa mazingira bado hazijafika na tunaliona hilo kama tatizo ambalo linaweza kutatuliwa pamoja ili kusogeza huduma hizo.

“Tunatiwa moyo sana na nia ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani, lakini kwa namna ambavyo tunaona na hasa katika sehemu za kutolea huduma na kufikisha maji nyumbani bado haijafikia asilimia 100,” amesema Mzinga.

Amesema licha ya huduma hiyo kutakiwa kuwa ya lazima kwa jamii, bado imekuwa vigumu kupatikana na wanaoathirika zaidi ni wanawake.

“Mtoto wa kike anapokuwa kwenye siku zake hawezi kuwa kwenye shule ambayo haina maji, choo safi na chenye mlango ambako anaweza kufanya huduma zake kwa usiri na kwa usafi.

“Suala la kutokuwa na maji na usafi wa mazingira linachangia katika kuwarudisha nyuma wanawake hata kiuchumi kwa sababu wanatumia muda mkubwa kwenye kutafuta maji,” amesema.

Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Shinyanga, Dk Christina Mnzava, amesema miongoni mwa majukumu yao ni kuhakikisha sera na mipango iliyopitishwa na Bunge inatekelezwa na Serikali.

“Sisi tunaotunga sera na sheria, kwa hiyo tuna wajibu mkubwa wa kuhakikisha zinatekelezwa. Sisi ndio tunaandaa bajeti, inapotengwa kwa ajili ya maji na usafi wa mazingira, tunahakikisha bajeti inapotengwa na kupitishwa tunafuatilia kama imefika kule inakotakiwa,” amesema.

Awali, akitoa mada katika mkutano huo, Christina Mhando kutoka Water Aid, amesema hadi mwaka 2021, kulikuwa na takribani vituo vya kutolea huduma za afya 8,549, lakini nusu ya vituo hivyo havina maji ya bomba na hata vilivyounganishwa na maji ya bomba havipati maji ya uhakika.

“Hadi asilimia 44 ya vyumba vya madaktari na asilimia 42 ya vyumba vya uzazi havina sehemu ya kunawia mikono ili kuwawezesha watoa huduma kufanya kazi kwa usafi.

“Hali hii inawaathiri watoa huduma walio mstari wa mbele kama wauguzi na wakunga na wanawake wakati wa kujifungua na wagonjwa wengine,” amesema.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts