KUELEKEA TAMASHA LA KIZIMKAZI MASHABIKI SIMBA,YANGA NUSURA WAZICHAPE VISIWANI ZANZIBAR

Na Said Mwishehe,Michuzi TV- Zanzibar

WAKATI wananchi wa Visiwa vya Zanzibar pamoja na Tanzania Bara wakijiandaa kushuhudia mchezo kati ya mashabiki wa Simba na Yanga inayotarajiwa kufanyika Kizimkazi visiwani hapa, mashabiki wa timu hizo wamejikuta wakiingia katika vita ya maneno nusura wazichape.

Mashabiki wa timu hizo kila mmoja amejinadi kuwa timu yake itaibuka mbabe na kunyakua kitita cha Sh.milioni tano pamoja na medali baada ya mwaka 2023 kukosekana mshindi,hivyo mwaka huu kila mmoja amejipanga kushinda mchezo huo.Wapenzi wa soka nchini na hasa wa timu hizo wanasubiria kuona nani ataibuka mbabe.

Mchezo wa mashabiki wa Simba na Yanga unayotarajiwa kuchezwa Agosti 17 mwaka huu ni sehemu ya kunogesha Tamasha la Kizimkazi ambalo limeandaliwa na Mwanamke Initiative Foundation chini ya Mwenyekiti wake Wanu Hafidh Ameir ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Wakizungumza leo Agosti 14,2024 katika vijiwe vya mashabiki wa Simba na Yanga walioko Makunduchi , mashabiki wa timu hizo wamesema wanatambua umuhimu wa mchezo huo na timu zao zimejipanga na kujiandaa kuonesha kandanda lililojaaa kila aina ya ufundi.

Shabiki maarufu wa Simba Miraji Maramoja na Mzaramu wamesema kuwa hawako tayari kuona wanapoteza mchezo huo na tayari na kwamba kikosi chao Kiko vizuri na kina uhakika wa kuibuka mshindi na kuchukua kitita cha Sh.milioni tano.

Kwa upande wake Miraji amesema kitu ambacho Yanga wanakiringia Simba wanakifahamu lakini akasisitiza kuwa katika mchezo huo Yanga hawatoki kwani watafungwa goli nyingi.

Wakati Mzaramu pamoja na kujigamba kuwa watashinda mchezo huo amempongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuhamasisha michezo nchini ukiwemo mchezo wa soka na kwamba amekuwa akitoa hamasa kubwa kwa timu zinazoshiriki michuano ya Klabu Bingwa na Shirikisho.

Hata hivyo wakati mashabiki wa Simba wakiwa katika mkutano wa kuzungumzia mchezo huo baadhi ya mashabiki wa Yanga wakiongozwa na Jimmy Kindoki pamoja na Teacher wa Yanga walivamia mkutano huo na kusababisha taharuki kiasi cha mabaunsa waliokuwa eneo hilo kuingilia kati baada ya kuona kuna kila dalili za kutaka kuzichapa.

Sababu za mashabiki wa Yanga kuvamia mkutano wa Simba ni baada ya mashabiki wa Simba nao kuleta vurugu katika mkutano wa Yanga hivyo mashabiki hao wakapanga kulipa kisasi na yote hiyo ni kuelekea katika mchezo huo ambao ni sehemu ya shamrashamra za tamasha kubwa la Kizimkazi Festival

Awali Jimmy Kindoki ambaye ni shabiki kindakindaki wa Yanga wakati anazungumzia mchezo huo amesema kuwa wanafanya hayo yote kwa lengo la kumuunga mkono Rais Samia na Mwanamke Initiative Foundation wamefanya kazi kuhakikisha mchezo huo unafanyika kama sehemu ya kuhamasisha michezo.

Kuhusu mchezo huo amesema Yanga hawana wasiwasi kwani wameizidi Simba kila nyanja kasoro umasikini lakini kwasababu ni Watanzania na wanaishi nao lazima wachangamane nao ili nao wawe na furaha kwani wanamwaka wa tatu hawajawahi kucheka yaaani kufurahi kwao wanasubiria Yanga ifanye vibaya jambo ambalo haliwezakani.

“Yanga tuko vizuri sana, tuko Bora na imefika wakati timu za Afrika kipimo chake ni Yanga.Simba wameona mapungufu yao baada ya kucheza na Yanga ndio wamegundua hawana Straika.Katika mchezo wetu na Simba tunakwenda na mfumo wa Gamond wa Gusa Unase lakini katika mchezo huu tunakwenda na mfumo Popo kanyeambingu.”

Ametumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania walioko nje ya Zanzibar ni vema wakafika katika tamasha la Kizimkazi kushuhudia mchezo huo na Yanga Wana uhakika wa kuchukua milioni tano maana utamaduni wao ni kuchukua makombe.





Related Posts