LIGI KUU SPESHO: Mechi hizi sio za kukosa

RATIBA ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025, imetolewa rasmi na Bodi ya Ligi (TPLB) huku kila timu ikitambua mpinzani itakayeanza naye mapema na itaanza kutimua vumbi Ijumaa hii ya Agosti 16, mwaka huu na kuhitimishwa Mei 24, mwakani.

Wakati ratiba inapotolewa kwa kila taifa lolote, jambo la kwanza linaloangaliwa ni michezo yenye hisia za mashabiki wa soka na hufahamika kwa maana ya ‘Dabi’ kutokana na ushindani baina ya timu zenyewe kwa sababu ya ukaribu wa makazi yao.

Kupitia makala haya, Mwanaspoti linakuletea michezo inayosubiriwa na wadau wengi wa soka kutokana na uhasama waliokuwa nao.

Hii ndiyo mechi inayosubiriwa kwa hamu kutokana na uhasama wa klabu hizi na ni moja ya ‘Dabi’ iliyojizoelea umaarufu ndani na nje ya nchi, huku zikiwa zimekutana mapema nusu fainali ya Ngao ya Jamii msimu huu na Yanga kushinda bao 1-0.

Simba ina kazi kubwa ya kulipa kisasi baada ya kupoteza michezo miwili ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita na ilianza na kichapo cha fedheha cha mabao 5-1, Novemba 5, 2023, kisha Aprili 20, mwaka huu ikaendeleza unyonge kwa kupoteza 2-1.

Msimu huu Simba itaanza wenyeji wa mchezo huu wa ‘Dabi ya Kariokoo’ ambao kwa ratiba ya awali unaonyesha utapigwa Uwanja wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam Oktoba 19, na ule wa marudiano ni Benjamin Mkapa Machi 1, 2025.

Mchezo mwingine utakaoteka hisia za wengi ni Yanga na Azam FC na msimu huu miamba hii inawakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kumaliza nafasi ya kwanza na ya pili.

Msimu uliopita kila timu ilishinda mchezo wake ikiwa mwenyeji na Yanga ilishinda mabao 3-2, Oktoba 23, mwaka jana kisha marudiano, Azam pia ikalipa kisasi baada ya kushinda 2-1, mechi ikipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Machi 17, mwaka huu.

Hata hivyo, miamba hii ilikutana katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la FA, msimu uliopita uliopigwa Uwanja wa New Amaan visiwani Zanzibar na Yanga ilitwaa ubingwa kwa penalti 6-5, baada ya kutoka suluhu ndani ya dakika 120.

Ratiba ya awali ya mchezo huu wa Ligi Kuu Bara baina ya miamba hii, bado haijapangiwa tarehe rasmi ingawa Yanga itakuwa mwenyeji katika mechi yake ya kwanza, huku ile ya marudiano itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ikichezwa Aprili 12, 2025.

Mchezo huu hutambulika kama ‘Dabi ya Mzizima’ na msimu uliopita Simba iliibuka kidedea kutokana na kutopoteza dhidi ya Azam FC.

Mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita, ilipigwa Februari 9, 2024, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na timu hizo kufungana bao 1-1, kisha marudiano Benjamin Mkapa Mei 9, 2024, Azam FC ikiwa mwenyeji ikachapwa mabao 3-0.

Licha ya Simba kutamba katika michezo yote miwili kwa msimu uliopita, ila Azam FC ndiyo iliyoinyima timu hiyo nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa msimu ujao na kujikuta ikidondokea kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.

Timu hizo zilikuwa na bato ya kugombea nafasi ya pili ili kukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa na ilibidi hadi michezo ya mwisho na Azam ikamaliza ya pili na pointi 69, sawa na Simba pia ila zilitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Msimu ujao timu hizi zitakutana mapema tu katika raundi ya nne ambapo hata hivyo ratiba inaonyesha mechi hii itapangiwa tarehe ya kuchezwa, ingawa marudiano ambayo Simba ndio itakuwa mwenyeji kwa Azam FC, zitakutana Februari 15, 2025.

Hii ni ‘Dabi ya Mbeya’ ambapo maafande wa Tanzania Prisons watakuwa na kibarua cha kupambana na wageni wa Ligi Kuu Bara KenGold.

KenGold iliyosota katika Ligi ya Championship kwa misimu mitatu mfululizo, imejihakikishia nafasi ya Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya kutwaa ubingwa huo kufuatia kumaliza kinara ikiwa na jumla ya pointi 70, katika michezo 30, iliyocheza.

Ushindi ilioupata wa mabao 2-0, dhidi ya FGA Talents mechi yake ya mwisho, iliifanya timu hiyo kukata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao ikiungana na Pamba Jiji ya jijini Mwanza iliyomaliza nafasi ya pili na jumla ya pointi zake 67.

Kwa misimu ya hivi karibuni, tumeshuhudia ‘Dabi ya Mbeya’ ikizikutanisha TZ Prisons na Mbeya City ingawa kwa sasa mambo yamebadilika, kwani City iliyoteka mashabiki wakati inapanda Ligi Kuu Bara mwaka 2013, inashiriki Ligi ya Championship.

Mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao baina ya miamba hii, Prisons itakuwa mwenyeji kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Novemba 8, mwaka huu, huku ile mechi ya marudiano ikitarajiwa kuchezwa uwanjani hapo hapo Aprili 11, 2025.

Huu utakuwa mchezo pia wa kuvutia kutokana na timu hizi ndizo zilizokata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao zikitokea Championship.

Katika Ligi ya Championship msimu uliopita, KenGold ndiyo ambayo ilitwaa ubingwa baada ya kukusanya jumla ya pointi 70, huku Pamba Jiji ikimaliza ya pili na pointi 67, jambo linaloonyesha wazi utakuwa mchezo wa kuvutia baina ya timu hizi.

Mchezo wa kwanza, utapigwa Desemba Mosi, mwaka huu na Pamba itakuwa mwenyeji wa KenGold kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, kisha marudiano miamba hii itakutana tena Mei 3, 2025, mechi itakayopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Pamba inayonolewa na Kocha Mkuu Mserbia, Goran Kopunovic, ina kibarua kigumu cha kuhakikisha inafanya vizuri katika Ligi Kuu Bara msimu ujao, kwani imepanda msimu huu baada ya kusota kwa miaka 23, tangu iliposhuka rasmi daraja mwaka 2001.

SINGIDA BS VS DODOMA JIJI

Hii ni ‘Dabi ya Kanda ya Kati’ itakayozikutanisha timu hizi ambapo mchezo wa kwanza Singida Black Stars itakuwa wenyeji wa Dodoma Jiji Uwanja wa CCM Liti Singida Desemba 12, na marudiano kupigwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma Mei 17, 2025.

Msimu uliopita katika michezo ya Ligi Kuu Bara ambayo timu hizi zilikutana, Singida ilikuwa mbabe kwani ilishinda yote miwili ikianza na ushindi wa mabao 2-1, Novemba 24, mwaka jana, kisha marudiano kushinda tena kwa 2-0, Mei 4, mwaka huu.

Hata hivyo, rekodi zinaonyesha Dodoma Jiji tangu mwaka 2022 ilipoanza kukutana na Singida haijawahi kushinda kwa sababu katika michezo minne ya Ligi Kuu Bara, imechapwa mitatu na kutoa sare mmoja tu jambo ambalo linasubiriwa kuona na msimu huu.

Related Posts