Lopez astaafu akikumbushia ya gwiji wa riadha

MICHEZO ya 31 ya Olimpiki iliyomalizika Jumapili iliyopita kule Paris, Ufaransa imeacha kumbukumbu mbalimbali za kihistoria zinazoingia kwenye vitabu kama zilizowekwa miaka mingi iliyopita ambazo zimekuwa hazisahauliki.

Mmoja kati ya wanariadha walioacha historia katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Ufaransa ni mwanamieleka wa Cuba, Mijain Lopez, ambaye alishinda medali yake ya tano ya dhahabu ya mieleka kwenye Olimpiki yake ya tano mfululizo kushiriki na kutangaza anastaafu.

Haikushangaza Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) ilipomchagua kuliwakilisha Bara la Amerika ya Kaskazini na wenzake wengine kwa mabara sita katika hafla kubwa ya kufunga michezo hiyo.

Lopez ambaye sasa ana umri wa miaka 41, amekuwa mwanariadha wa kwanza katika historia ya michezo yote kiujumla kushinda medali tano mfululizo za Olimpiki za mchezo mmoja, akitwaa moja kila aliposhiriki michezo hiyo ndani ya kipindi cha miaka 20.

Mbali ya kushinda medali 5 za dhahabu za Olimpiki, Lopez pia ni mshindi medali tano za dhahabu za mashindano ya Mabingwa wa Dunia, medali tano za dhahabu za Michezo ya Pan American.

Baada ya kumchapa Yasmani Acosta wa Chile katika fainali ya pambano la mieleka la uzito Kg 130 kwenye Olimpiki ya Paris 2024, Lopez alivua viatu vyake alivyovitumia kushinda na kuviacha katikati ya ulingo kama ishara ya kustaafu mchezo huo.

Mafanikio ya Lopez yaliwakumbusha zaidi ya watu 71,000 waliofurika kwenye Uwanja wa Taifa wa Ufaransa, Stade de France, umahiri kama huo ambao alikuwa nao mwanariadha wa Finland, Paavo Rumi (13 Juni 1897 –2 Oktoba 1973).

Paavo Nurmi alijuliana kama the ‘Flying Finn’ (Raia wa Finland anayeruka). Huyu ni mwanariadha aliyeng’ara katika michezo ya 1920 iliyofanyika Antwerp, Uholanzi kwa kunyakuwa medali tatu za dhahabu.

Hii ilikuwa katika mbio za mita 10000, mbio za nyika za mtu mmoja mmoja na za nchi na medali ya fedha katika mbio za mita 5000 katika kipindi cha siku tatu.

Vile vile katika michezo hii iliyofanyika Paris, Ufaransa miaka minne badaye alishinda mbio za mita 1500 na saa tatu baadaye alichukua medali ya dhahabu ya mbio za mita 5000.

Katika michezo hii iliyofanyika Amsterdam, Uholanzi, mwaka 1928, Nurmi alichukua medali ya dhahabu ya mita 10000 na fedha, mita 5000 na mbio za mita 3000 zinazohusisha kuruka viunzi na kutua kwenye maji (steeplechase).

Kwa ujumla alishinda medali 9 za dhahabu.

Paavo Johan Paavo Nurmi, kijiji cha Turku, Finland, aliheshimika kwa kuendeleza ushindani katika michezo ya Olimpiki kwa kutawala kila mchezo alioshiriki tangu akiwa na umri wa miaka 22 mwaka 1920.

Nurmi mwenye urefu wa sentmita 174 na uzito wa kilo 65 alikuwa mkimbiaji mwenye mbinu na wakati wote alipokimbia aliangalia mbele na kuonekana hajali aliokimbia nao wawe pembeni au nyuma

Vilevile alishiriki katika mashindano ya ndani ya uwanja kama kuruka, kurusha tufe, mkuki na mengine. Nurmi alianza kupata umaarufu tarehe 29 Mei 1920 alipoweka rekodi ya taifa ya Finland ya mbio za mita 3000 kwa kutumia dakika 8 na sekunde 36.2 na alipomaliza akazunguka uwanja mzima kwa mwendo wa kasi huku akiwapungia watazamaji.

Baada ya hapo alianza kuvunja rekodi za dunia moja baada ya nyingine, wakati mwengine katika kipindi cha wiki moja, kuanzia ya mbio za mita 1,5000 na zikafuata hadi za mita 10,000.

Katika michezo ya 8 ya Olimpiki iliyofanyika Paris mwaka 1924 (miaka

100 iliyopita) Nurmi alipata medali tano za dhahabu katika kipindi cha siku sita na mbili kati ya hizo alizipata baada ya mapumziko ya chini ya saa mbili.

Gazeti maarufu la michezo la Ufaransa, Miroir des Sports liliandika: “Paavo Nurmi sio binadamu wa kawaida. Au wapo wawili ambao ni pacha na tunashindwa kutambua na kudhani ni huyohuyo mtu mmoja?”

Katika mwaka 1925 Paavo Nurmi alitembelea Marekani kwa miezi mitano.

Akiwa huko alishiriki mashindano ya masafa tofauti mara 53 na kushinda yote.

Siku moja wakati akipokea zawadi aliwaambia walioandaa mashindano wakimwita mara nyingine basi washiriki wenzake wapewe kitambo, yaani wawe angalau mita moja mbele yake kwa mashindano ya masafa ya kati na mita tatu hadi nne kwa mbio za maafa marefu wakati wa kuanza kukimbia.

Tangu akiwa kijana mwanzoni mwa miaka ya 1920, Nurmi aliwekeza katika biashara na hasa ujenzi wa nyumba. Katika jiji la Helsinki alimiliki nyumba 40.

Mashindano ya mwisho ya Paavo Nurmi yalikuwa ni ya ushindi wa mbio za mita 10,000 huko Viipuri, Finaland Septemba 16, 1934.

Hata baada ya mwanariadha huyo jasiri wa Finland kustaafu, bado alijihusisha na riadha kwa kujitokeza mara nyingi kuwapa mafunzo vijana na mwanzoni mwa mwaka 1940 alikwenda Marekani kuchangisha fedha za kuisaidia nchi yake ambayo ilikuwa inapigana vita na Urusi.

Finland ilipokuwa mwenyeji wa michezo ya 15 ya Olimpiki mwaka 1952 mtu aliyeingia uwanjani na mwenge wa Olimpiki alikuwa ni Nurmi.

Alipofariki dunia mwaka 1973 habari zake na mazishi yake ya kitaifa yalitangazwa sana kila pembe ya dunia na amejengewa sanamu katika mji aliozaliwa wa Turku.

Vilevile, vipo vitabu na michezo ya sinema inayoelezea maisha yake ndani nje ya uwanja wa michezo. Pia Benki ya Finland iliwahi kutoa noti zenye picha ya mwanariadha huyu wa Finland.

Si ajabu jina lake likaendelea kukumbukwa kila inapofanyika michezo ya Olimpiki popote pale duniani siku zijazo.

Related Posts