Lukuvi, Kabudi warejeshwa Baraza la Mawaziri, Ummy, Kairuki wang’olewa

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi na uhamisho wa viongozi mbalimbali, wakiwemo William Lukuvi na Profesa Palamagamba Kabudi ambao wamrejeshwa kwenye Baraza la Mawaziri.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Moses Kusiluka, pamoja na wawili hao viongozi walioteuliwa na kuhamishwa vituo vya kazi ni kama ifuatavyo:

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Sharifa Nyanga, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema Profesa Kabudi ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, huku Lukuvi akiteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).

Taarifa hiyo iliyotolewa leo Agosti 14, 2024 imesema Jenista Mhagama ameteuliwa kuwa Waziri wa Afya kuchukua nafasi ya Ummy Mwalimu, kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).

Pia amemteua Balozi Pindi Chana kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, awali alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Anachukua nafasi ya Angellah Kairuki, aliyeteuliwa kuwa Mshauri wa Rais.

Rais Samia pia ameteua Hamza Johari kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuchukua nafasi ya Jaji Eliezer Feleshi, ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.  Kabla ya uteuzi huo Johari alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

Samwel Maneno, ameteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, awali alikuwa Msaidizi wa Rais, Sheria. Anachukua nafasi ya Balozi Kennedy Gastorn ambaye ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais, Sheria na Mikataba.

Mteule mwingine ni Dk Ally Possi ambaye anakuwa Wakili Mkuu wa Serikali, kabla ya uteuzi alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi.

Mbali ya hao, Rais Samia pia ameteua  Salum Hamduni kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). Hamduni anachukua nafasi ya Profesa Siza Tumbo ambaye amerejea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Rais pia amemteua Ismail Rumatila kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, awali alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Mwingine aliyeteuliwa na Rais ni Atupele Mwambene anayekuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia masuala ya elimu. Kabla ya uteuzi alikuwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Rais Samia amemteua Abdul Mhinte kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia mifugo. Kabla ya uteuzi alikuwa Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu.

Pia Methusela Ntonda ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu.

Uhamisho wa naibu makatibu wakuu

Dk Grace Magembe amehamishwa kutoka Wizara ya Afya kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia masuala ya afya.

Dk Charles Msonde amehamishwa kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, huku Dk Wilson Charles amehamishwa kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, anayeshughulikia masuala ya elimu ya msingi na sekondari.

Profesa Daniel Mushi amehamishwa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia masuala ya sayansi na elimu ya juu.

Dk Franklin Rwezimula amehamishwa kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, huku Dk Khatibu Kazungu amehamishwa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya umeme na nishati jadidifu.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts