Mawakala wa forodha walia na mfumo hodhi wa manunuzi serikalini

Dar es Salaam. Chama cha Wakala wa Forodha Tanzania (Taffa) kimeeleza kuwa uamuzi wa Serikali kutumia Wakala wa Huduma na Ununuzi Serikalini (GPSA) katika manunuzi yote unawakosesha kazi na kuathiri shughuli zao za kila siku.

Kutokana na hilo, kimemuomba Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa awasaidie mawakala kwa kurejesha uhai wa shughuli zao kupitia ushindani.

Hayo yamesemwa leo, Agosti 14, 2024, na Rais wa Taffa, Edward Urio, wakati wa ufunguzi wa kongamano la kimataifa la siku tatu la uchukuzi linalofanyika jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo limeandaliwa na Shirika la Mawakala wa Forodha Afrika Mashariki (Feaffa) na kuratibiwa na Taffa.

Urio amemtaka Waziri Mbarawa aingilie kati uhodhi wa kazi za uchukuzi za taasisi za Serikali na miradi ya Serikali, unaofanywa na GPSA bila kuzingatia sheria ya ushindani.

Amesema wanafahamu kuwa suala hilo halikukusudiwa kwa nia mbaya, lakini Serikali na Watanzania watapata huduma bora na thamani ya fedha ikiwa itanunua huduma kwa ushindani, kwani itafungua fursa katika tasnia na kuiwezesha Serikali kunufaika na ufanisi utakaopatikana.

Amesema utaratibu uliopo sasa unaoifanya GPSA kuwa wakala wa pekee wa mizigo ya Serikali, taasisi zake, na miradi mikubwa umefanya baadhi ya wanachama wa Taffa kukosa biashara.

Ametolea mfano wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambalo lina takribani miradi 1,000 ambayo wakandarasi wamekuwa wakiomba zabuni kwa ajili ya maendeleo.

“Wakandarasi hawa kwenye mchakato wa kuandaa gharama za mradi, suala la usafirishaji mizigo anapewa mkandarasi. Ila kwa sababu ni miradi ya Serikali na kuheshimu sera ya misamaha ya kodi, analazimika kutumia jina la Tanesco ili aweze kupita wizarani na kupata misamaha,” amesema Urio.

Amesema mwisho wa siku, utekelezaji wa mambo yote katika masuala ya usafirishaji ikiwa kutakuwa na ucheleweshaji wa mradi, mkandarasi ndiye anahusika katika kujibu.

“Kwa sasa tumeshuhudia wingi wa miradi ya kimaendeleo iliyopo awamu ya sita. Kurundika kazi zote za taasisi za Serikali kwa GPSA, kutazidi kuongeza gharama kwenye miradi yetu,” amesema Urio.

Takwimu zinaonyesha, wakati Tanesco inaruhusu wakandarasi kutafuta mawakala wa forodha wenyewe, ilikuwa ikitoa barua za idhinisho kwa zaidi ya mawakala wa forodha 300 kwa sababu kila mradi na mkandarasi alikuwa na wakala wake. Hii ilikuwa fursa kwa wanachama wa Taffa ambao ni zaidi ya 1,000, na kuwafanya kufurahia fursa za miradi ya Serikali na kuchangia pato la Taifa la Serikali kwa kwenye kodi na kuzalisha ajira.

“Ni imani yetu, chini ya Serikali ya awamu ya sita chini ya wizara yako, ile neema uliyotufanyia katika kuboresha Sheria ya TASAC, wanachama wamenituma nikuombe ukawe balozi wetu ili kutusaidia na kukuza uchumi wa wana tasnia waweze kushindana katika soko la Afrika na SADC, ambalo Tanzania ni mwanachama wake,” amesema Urio.

Hata hivyo, ametumia nafasi hiyo kupongeza hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kufanya mapitio ya sheria ya Wakala wa Reli Tanzania (TASAC), ambayo imesaidia kufungua fursa kwa wanachama wa Taffa.

Amesema Tanzania ni kitovu cha usafirishaji kutokana na kuwa na bandari nyingi, ikiwemo bandari za maziwa makuu, anga na barabara.

Hivyo ni vyema kuhakikisha kunakuwa na uhusiano mzuri kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Akijibu hoja ya GPSA, Waziri wa Uchukuzi amesema wamepokea mapendekezo yaliyotolewa na kuelekeza kama mengine yapo yawasilishwe ili kuangalia namna ya kuyafanyia kazi.

Profesa Mbarawa amesema Serikali imejipanga kuendelea kukamilisha miradi yote ili kuhakikisha huduma za uchukuzi na usafirishaji zinafanyika bila vikwazo.

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa amesema Tanzania inatarajia kupokea ndege mpya aina ya Boeing 787-8 (Dreamliner) wiki ijayo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar (AAKIA), ikiwa ni miezi michache tangu ndege nyingine aina ya Boeing B737-9 Max kupokelewa Machi 26 mwaka huu.

 Ndege hiyo itakuwa ya 14 kununuliwa, ambapo kati ya 13 zilizopo hadi sasa moja ni ya mizigo. Ndege hizi zinafanya safari zake kikanda, kimataifa na ndani ya nchi.

Profesa Mbarawa amesema uingizwaji wa ndege hii ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuboresha uwekezaji katika Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL). “Hadi Novemba mwaka jana, Serikali ilikuwa imenunua na kupokea ndege 13 mpya, ikiwemo moja ya mizigo zinazofanya kazi kikanda na kimataifa.

Profesa Mbarawa amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma zote za usafiri na usafirishaji nchini na kuondoa vikwazo vyote.

Related Posts