Mbarawa: Tunataka SGR ifanye kazi saa 24

Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema wamejipanga kushirikiana na sekta binafsi katika utekeleza miradi mbalimbali kwa utaratibu Ushirikiano wa Serikali na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP).

Katika kufanikisha hilo, Profesa Mbarawa amesema Serikali imefanya marekebisho ya sheria ya Reli namba 10 ya mwaka 2017 ili kuruhusu ushiriki wa sekta binafsi katika utoaji huduma kwa njia ya reli.

“Hivyo, pamoja na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutoa huduma za treni, sekta binafsi inakaribishwa kutoa huduma hizo ili kuhakikisha wateja wananufaika na miundombinu iliyojengwa,” amesema Profesa Mbarawa.

Waziri huyo amesema hayo leo Jumatano, Agosti 14, 2024 wakati akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la kimataifa la siku tatu la uchukuzi  linalofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema mdau yeyote anakaribishwa kuja na mabehewa na vichwa ili aweze kufanya shughuli zake katika reli ya kisasa.

“Mnaweza kujipanga ninyi watu kumi, mkaenda kununua vichwa kumi, tunawapa muda wenu mnaendesha treni zetu, tunataka treni ile ifanye kazi saa 24 kwa siku, ifanye kazi asubuhi, mchana, jioni, usiku na usiku wa manane, tukifanya hivyo tutaona mabadiliko makubwa ya uchumi, fursa ipo ni ninyi kujipanga kuitumia,” amesema Profesa Mbarawa.

Amesema wanaweza kuleta wadau wengine kutoka nje kwani milango iko wazi baada ya sheria kubadilishwa na kuandikwa kanuni zinaoweka wazi fursa.

“Hatutaki kila kitu kibaki kwa TRC, tunaamini TRC pekee haitaweza kutoa huduma kubwa kama hiyo, tunaamini tukitoa fursa kwa sekta binafsi tutaona mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri na usafirishaji,” amesema

Amesema suala hilo litashusha hata gharama za usafirishaji wa mizigo kwani muda wa kusafirisha mzigo kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma utapungua kutoka saa 10 hadi 5, hivyo kufanya bei zipungue.

Related Posts