Mkojo kutumika kubaini vimelea vya kifua kikuu kwa watoto

Dar es Salaam. Kutokana na ugumu wa kuwabaini watoto walioambukizwa Ugonjwa Kifua Kikuu (TB), Serikali imetangaza teknolojia mpya ya kuchunguza vimelea vya ugonjwa huo kupitia mkojo.

Kinachosubiriwa kuanza kutumikia kwa teknolojia hiyo ni vitendanishi vitakavyowezesha upimaji wa mkojo kwa watoto ili kubaini maambukizi ya kifua kikuu.

“Tumeleta teknolojia ya uchunguzi wa vimelea vya kifua kikuu kwa watoto kupitia mkojo, hii itakuwa suluhisho ya changamoto ya kubaini watoto wenye kifua kikuu,” amesema Mkuu wa Programu, Wizara ya Afya, Dk Catherine Joachim.

“Utambuzi wa kifua kikuu kwa watoto ni mgumu kwa sababu ugonjwa huu hupimwa makohozi na kupitia X-Ray, hivyo njia hizo ni ngumu kwa watoto.”

Dk Joachim amesema hayo leo Jumatano Agosti 14, 2024 katika mkutano wa kupitia taarifa ya viashiria vya magonjwa ya ngono, kifua kikuu, malaria na ukoma.

Mkutano huo wa nusu mwaka umeandaliwa kwa ushirikiano na Mpango wa Taifa Kudhibiti Malaria (NMCP), Mpango wa Taifa Kudhibiti Ukimwi (NTLP) na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (NASHCOP).

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, kuanzia mwaka 2018 hadi 2022 wagonjwa wa kifua kikuu walioibuliwa ni 400,031, kati yao watoto ni 67,000.

Amesema katika kukabiliana na kifua kikuu kuanzia ngazi ya msingi hadi hospitali ya rufaa ya mkoa, Serikali itasambaza mashine za kubaini vimelea vya ugonjwa huo na itawatumia watoa huduma ngazi ya jamii kufuatilia wagonjwa wapya.

Mbali ya hatua hiyo, amesema wameanzisha jukwaa linalojumuisha sekta zenye wagonjwa wengi wa kifua kikuu, hasa za madini na uvuvi lengo likiwa kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo.

“Changamoto tuliyonayo sasa ni kuibua wagonjwa wapya kwenye makundi hatarishi, usugu wa dawa dhidi ya vimelea na wigo wa utoaji huduma katika vituo binafsi vya afya kuwa mdogo, ni asilimia 12 pekee ya wagonjwa wamegunduliwa kupitia hospitali binafsi,” amesema.

Awali, akifungua mkutano huo, Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Rashid Mfaume amesema jitihada zinazofanywa sasa na Serikali ni utambuzi wa wagonjwa wapya wa kifua kikuu.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zenye idadi kubwa ya wagonjwa wa kifua kikuu takwimu zikionyesha kwa kila watu 100,000 watu 195 wanabainika kuwa na kifua kikuu,” amesema.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha watu wanaopoteza maisha kutokana na ugonjwa huo kwa siku ni 70 na wengine 25,800 hupoteza maisha kwa mwaka kwa maradhi ya kifua kikuu.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha watu milioni 10.6 walioambukizwa kifua kikuu duniani, wanaume ni milioni 5.8, wanawake milioni 3.5 na watoto milioni 1.3
Kuhusu maambukizi ya Ukimwi, Dk Mfaume amesema katika utekelezaji wa malengo ya dunia ya kudhibiti maambukizi ya Ukimwi 95, 95,95 yaani asilimia 95 ya wenye Virusi vya Ukimwi (VVU) wawe wanatambua hali zao na asilimia 95 ya wanaotambua hali zao wawe wameanza dawa na asilimia 95 ya walioanza dawa wawe wamefubaza maambukizi;  changamoto ipo kwa vijana na watoto.

Amesema makundi hayo mawili hayajitokezi kupima na kupata dawa hatua iliyoifanya Serikali kuwaomba wadau kuendelea kushirikiana kukabiliana na tatizo hilo.

Meneja wa Taifa wa Mpango wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini, Dk Prosper Njau amesema zipo hatua zilizofikiwa katika utambuzi wa watu wanaoishi na VVU.

“Mwaka 2016 kulifanyika utafiti nchini na kubaini asilimia 60 ya wenye maambukizi wanatambua hali zao na asilimia 94 walikuwa kwenye dawa, asilimia 87 walifubaza maambukizi.

Mwaka 2022-2023 ulitoka utafiti mwingine na kuonyesha asilimia 83 ya wenye maambukizi wanafahamu hali zao na asilimia 98 ya wanaotambua hali wapo kwenye dawa na asilimia 95 wamefubaza maambukizi,” amesema.
Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Dk Samwel Lazaro amesema kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo nchini ni asilimia 8.1 tofauti na miaka 1990, yalikuwa asilimia zaidi ya 50.

Licha ya uwepo wa mafanikio hayo ya muda mrefu Dk Lazaro amesema ipo mikoa ambayo kiwango cha maambukizi kipo juu ikiwamo Tabora, Mtwara, Kagera, Shinyanga na Mara.

“Serikali itaendelea kuchukua hatua kudhitibi malaria katika mikoa yenye viwango vya juu ya maambukizi, kwa mwaka huu 2024/2025 Serikali imetoa Sh11 bilioni kutekeleza afua za unyunyiziaji dawa maeneo yanayokaa viluilui kwa halmashauri 57 zenye kiwango cha juu cha maambukizi,” amesema.

Kuhusu ukoma ambao huambukizwa kwa njia ya hewa, Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma, Dk Riziki Kisonga amesema katika kukabiliana na ugonjwa huo, wataalamu wanapomuibua mgonjwa ndani ya familia, uchunguzi hufanyika kwa familia nzima.

“Ugonjwa huu unatibika na kwa mwaka tunaibua wagonjwa 1,500, mikoa yenye idadi kubwa ya wagonjwa ni Dodoma, Morogoro, Lindi na Tanga na halmashauri za Ifakara, Lindi na Mtwara,” amesema.

Ili Serikali iendelee kuchukua hatua kudhibiti magonjwa hayo, Mwenyekiti na Mwakilishi wa Jamii inayopambana na Magonjwa Tanzania (Conamet), Gesongo Paul amesema wataendelea kupaza sauti kuhusu magonjwa yanayoathiri jamii ili yashughulikiwe. 

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts