Dar es Salaam. Uelewa hafifu kwa jamii juu ya athari za kimazingira na kiafya zitokanazo na matumizi ya vifungashio vya plastiki, ni moja ya sababu zinazotajwa kuchangia kuendelea kuzalishwa kwa siri kwa kuwa wanaangalia upande wa faida pekee.
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limesema changamoto hiyo ni moja ya kikwazo kikubwa wanachopitia katika kukomesha uzalishaji, usambazaji na matumizi yake kwa ujumla nchini.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Agosti 14, 2024 na Meneja wa NEMC, Kanda ya Temeke, Arnold Mapinduzi katika semina ya mazingira kwa Kikundi cha Wanawake na Samia kutoka wilaya tano za Mkoa wa Dar es Salaam.
Amesema kwa kutambua hilo, wamejipanga kutoa elimu endelevu hadi ngazi za chini katika mapambano hayo ili jamii ielewe.
“Mwaka 2019 Serikali ilipiga marufuku matumizi ya vifungashio vya plastiki, imekuwa ngumu kukomesha kwa kuwa bado watu wanatumia, lakini tunaamini jamii ikielewa athari zake kwa kina itakuwa rahisi kukomesha.
“Serikali ilipiga marufuku kwa kuwa inapenda watu wake kwa kutambua mazingira ni afya na uhai. Ndani ya plastiki kuna kemikali inayofanya kifungashio hicho kisipitishe maji na hewa, ili kulinda kilichofungashwa lakini ni hatari kwa afya ya binadamu,” amesema.
Mapinduzi amesema adui mojawapo wa plastiki ni joto, kwani ikichomwa inaruhusu ile joto inaachia na inakuwa na athari kwa afya, hivyo kushauri watu warudie mfumo wa asili wa zamani wa kubeba bidhaa kutoka sokoni kwa kutumia vifungashio vingine vinavyokubalika kwa usalama wa afya.
“Kukosa elimu watu wanatumia mifuko hiyo kuwekea vyakula na wengine kupikia vyakula kama wali na ugali, jambo ambalo ni hatari na inakuwa chanzo cha kupata magonjwa mbalimbali ikiwemo kansa,” amesema.
Pia Mapinduzi amesema kupitia semina hiyo, wamewaelekeza umuhimu wa kutoa taarifa kwa mkurugenzi wa halmashauri husika na wakiona hatua hazijachukuliwa wanapaswa kuwasilisha taarifa hizo NEMC watakaojua cha kufanya.
Kwa upande wake, mwenyekiti na kiongozi wa kikundi hicho, Sofia Kinega amesema baada ya kupata elimu na kutambua athari zake watakuwa mabalozi wazuri katika kuhakikisha wanakomesha matumizi ya vifungashio.
“Leo tumezaliwa upya, tulikuwa tunajiona tunajua kumbe hatujui tunatumia plastiki hata katika kuwasha moto, ili tupike kwa kuwa tulikuwa hatujui madhara yake,” amesema Sofia.
Akizungumza katika semina hiyo, katibu wa idara ya mazingira katika kikundi hicho, Hanifa Mrisho amesema katika utoaji elimu ni muhimu NEMC kushirikiana na Serikali za mitaa kuwafikia watu wengi hasa wanapoanzisha kampeni.