NMB kumkabidhi Rais Samia shule, maadhimisho Tamasha la Kizimkazi

Unguja. Wakati kamati ya maandalizi ya tamasha la Kizimkazi mwaka 2024 ikitambulisha wadhamini wa mwaka huu, Benki ya NMB, imejipanga kuwanoa wajasiriamali zaidi ya 700.

Pia, inatarajiwa kukabidhi Shule ya Maandalizi ya Tasani, iliyoko Makunduchi Zanzibar.

Tamasha hilo litatumika kuzindua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na wadau wa maendeleo, zikiwemo taasisi binafsi.

Tamasha hilo litazinduliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, miradi ya zaidi ya Sh5 bilioni ikitarajiwa kuzinduliwa.

Akizungumza wakati wa utambulisho wa wadhamini hao, Meneja wa Biashara wa NMB Zanzibar, Naima Said Shaame, amesema benki hiyo itashiriki kwa sehemu kubwa katika tamasha hilo ili kuchochea maendeleo.

“Tunalichukulia tamasha hili kwa ukubwa na umuhimu wake, tumekuwa bega kwa bega na tamasha hili tangu linaanzishwa, tuko nalo na tutaendelea nalo, lakini kwa mwaka huu niseme kama ukubwa wa benki yetu ulivyo, basi ushiriki wetu utakuwa mkubwa pia,” amesema.

“NMB tunathamini, tunajali na kupambania uchumi wa mtu mmoja na Taifa kwa ujumla, tuko hapa kudhamini Kizimkazi Festival kwa sababu ni tamasha linalotumika kunyanyua uchumi na pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” amesema.

Naima amesema NMB itafanya mambo makuu matatu, la kwanza ni mafunzo kwa wajasiriamali zaidi ya 700 ambao watanolewa juu ya elimu ya fedha, uwekezaji na uimarishaji wa shughuli zao za kijasiriamali.

Pia, kutakuwa na uzinduzi na kukabidhi Shule ya Maandalizi ya Tasani, ambayo itakabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ndiye aliyeweka jiwe la msingi Agosti 29, 2023.

Shule hiyo inajumuisha madarasa matano yatakayochukua wanafunzi 200, sawa na wanafunzi 40 kila moja, ofisi ya mwalimu mkuu, ofisi ya walimu, wafanyakazi, stoo, mifumo ya kisasa ya majisafi na majitaka na sehemu ya michezo.

Mwenyekiti wa Tamasha la Kizimkazi, Mahfudh Said Omar, amemtangaza mhamasishaji Dotto Magari kuwa balozi wa tamasha la mwaka huu.

Amesema kila mdhamini atakuwa na siku za utekelezaji wa majukumu ya kimkataba, lengo likiwa ni kutoa fursa pana kwa wawezeshaji.

Related Posts