Othman ataja maeneo saba ya kurekebishwa kabla uchaguzi mkuu 2025

Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud ametaja maeneo saba yanayohitaji kufanyiwa marekebisho haraka kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Mambo hayo ni haki ya kisheria ya kuwapatia wananchi vitambulisho vya Mzanzibari (Zan ID), uandikishaji wa haki ndani ya daftari la kudumu la wapigakura (PVR), kuondoa na kudhibiti wapigakura mamluki pamoja na kuepusha udanganyifu kupitia uchaguzi wa siku mbili Zanzibar.

Mengine ni kuwepo tume huru ya kusimamia demokrasia, uchaguzi wa haki na kuheshimu maamuzi ya wananchi kupitia sanduku la kura na kuachana na matumizi ya vikosi vya ulinzi na usalama.

Hayo yamo katika taarifa ya Agosti 13, 2024 iliyotolewa na kitengo cha habari, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwenda kwa vyombo vya habari.

Othman ametoa kauli hiyo Agosti 13, ofisini kwake Mazizini alipozungumza na ujumbe kutoka ubalozi wa Marekani nchini ulioongozwa na Naibu Balozi wa Taifa hilo Tanzania, Andrew Lentz.

“Ili kuifanya Zanzibar na Wazanzibari kurudisha imani yao kwa Serikali na mamlaka zinazotawala, lazima kuondoa hofu na mifumo dhalimu ya uchaguzi, hakuna namna zaidi ya kuwa na dhamira njema ya kisiasa na kutekeleza demokrasia kwa vitendo bila kufanya hivyo,” amesema Othman.

Amesema tangu kuwapo kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1995, Zanzibar imekuwa na uchaguzi unaoacha vilio na makovu jambo ambalo halileti afya njema kwa mustakabali wa amani na maendeleo ya Taifa kwa jumla.

Amezungumzia uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 akisema watu 21 walipoteza maisha na wengine 38 kuachwa na ulemavu wa kudumu.

Kuhusu kuimarisha uchumi wa nchi, Othman amesema Zanzibar inahitaji uwajibikaji na uwazi ili kufungua fursa za uwekezaji kutoka nje, huku akisisitiza siku zote mwekezaji huwekeza fedha zake katika eneo lenye amani.

Ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali ya Marekani kuendelea kutoa ushirikiano kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika kufanikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, utakaoiwezesha kujitegemea na kuongeza kasi ya maendeleo, na kusaidia utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Buluu.

Amebainisha uwepo wa fursa nyingi za kiuchumi iwapo vijana watajengewa uwezo katika uvuvi, kilimo na ufugaji, akieleza wataweza kujiajiri na kusaidia kuongeza pato la Taifa.

Balozi Lentz ameahidi kuendeleza ushirikiano kati ya Marekani na Zanzibar, akisisitiza umuhimu wa wananchi kupata ithibati juu ya imani na amani yao kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Amesema akiwa Zanzibar na ujumbe wake, pamoja na mambo mengine wamekuwa na mazungumzo na vijana kadhaa, ambao baadhi wameonyesha hofu juu ya viashiria vya kile ambacho kinaweza kujiri katika uchaguzi huo.

Amesema Marekani itaendeleza ushirikiano huo wa muda mrefu katika vipaumbele vya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, miundombinu, utawala bora na uwajibikaji.

Related Posts