PAMBA Jiji maarufu kama TP Lindanda ‘Wana Kawekamo’ wanarudi Ligi Kuu baada ya miaka 23 tangu waliposhuka daraja mwaka 2000, na Ijumaa itacheza mchezo wake wa kwanza wa michuano hiyo itakapofungua pazia la Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Pamba ni miongoni mwa timu zenye umaarufu na historia kubwa nchini mbali ya Simba na Yanga, ikiwa imeshatwaa ubingwa wa Tanzania mwaka 1990 na kutoa wachezaji mahiri akiwemo Madata Lubigisa, Joram Mwakatika, Fumo Felician, George Masatu, David Mwakalebela, Kitwana Seleman, Hussein Marsha na Paul Rwechungura.
Pamba Jiji ambayo inamilikiwa na halmashauri ya Jiji la Mwanza imesuka safu mpya ya uongozi, na benchi la ufundi linaloongozwa na Goran Kopunovic, Salvatory Edward na Razack Siwa huku ikitengeneza kikosi cha wachezaji 26 wakiwemo nyota wapya 19 na wa zamani saba.
Katika kuhakikisha inakwepa jinamizi la timu ngeni kwenye Ligi Kuu kupata wakati mgumu na kupigania kubaki Ligi Kuu ama kurudi zilipotoka, Viongozi na benchi la ufundi wamejipanga kufanya vizuri na kuhakikisha wanaendelea kuwepo ili kuwapa furaha mashabiki na Wana Mwanza baada ya kipindi kirefu kupita.
Kocha huyu mkuu wa kikosi hicho ambaye msimu uliopita alikuwa na Tabora United kwenye Ligi Kuu, anasema amejaribu kuunda kikosi chenye wachezaji wengi vijana na wenye vipaji ambao watacheza soka la kisasa lakini akatahadharisha mashabiki kutokuwa na matarajio makubwa kwani anahitaji muda.
Anasema timu inayopanda Ligi Kuu anapata mtihani mkubwa kuzoea na kuhimili ushindani, hivyo wanapaswa kuwa na tahadhari na mashabiki hawapaswi kukata tamaa mapema pale timu inapopoteza bali waiunge mkono wakati wote.
“Tunapambana kila siku tunajituma kutengeneza timu ya ushindani, klabu inataka kumaliza nafasi nne za juu lakini mimi sipendi ahadi na sitaki kuahidi mambo makubwa nahitaji tu kila mtu awe na subira tutasherehekea mwisho wa msimu,†anasema Kopunovic
“Kwa timu mpya inayoingia Ligi Kuu ni mtihani mkubwa na ni ngumu kwahiyo tunapaswa kuwa makini tuwe na timu ya kushindana na tucheze soka la kisasa ili tuibakishe timu Ligi Kuu, lazima twende hatua kwa hatua na mashabiki waiunge mkono timu yao,â€
“Tuko kwenye mwelekeo sahihi tunatakiwa kuwa na subira, kuamini na kufanya kazi kwa bidi kila mchezaji anapaswa kujiamini na kuonyesha nia ya kufanya vizuri alafu benchi la ufundi litaamua nani aanze,†anasema.
Kocha wa makipa, Razack Siwa anasema ana imani na eneo lake la kipa ambalo linaongozwa na Shaban Kado, Yona Amos na wengine chipukizi wawili, huku akiamini kama watafuata maelekezo yake basi watafanya vizuri na kuisaidia timu hiyo kuhimili vishindo vya Ligi Kuu.
“Mimi napenda mtu mwenye bidi na wengi nilionao wanajituma nategemea kupata makipa wazuri kwa sababu wanafanyia kazi maelekezo ninayowapa. Kipa akiweza kujituma, kujisahihisha anapokosea na kuheshimu ninachokifanya ni rahisi kumsaidia kuwa kipa bora,†anasema Siwa
Nahodha wa timu hiyo, Shaban Kado anasema kikosi chao kilipata maandalizi mazuri kwa takribani wiki tano na kupata ulivu, maelewano na umoja miongoni mwa wachezaji, hivyo, wamejiandaa kufanya vizuri na kuhakikisha hawarudii makosa ya timu nyingi zinazopanda daraja.
“Tuna kikosi kipana karibu kila nafasi ina wachezaji kuanzia wawili ambayo yanampa machaguo mengi mwalimu lakini yeyote atakayepata nafasi anaipambania Pamba. Tumeona ratiba yetu Ligi Kuu tuna muda na nguvu ya kutosha,â€
“Sisi tumejiandaa kushinda mechi zote ili tuwe sehemu salama, maandalizi ya mechi zetu tatu za kwanza nyumbani yameshapangwa na tunataka tushinde na kufanya vizuri ili tuwe na mwanzo mzuri kwenye Ligi Kuu na kuhakikisha tunaendelea kuwepo,†anasema Kado
Kinara wa mafanikio ya Pamba Jiji na aliyekuwa Mlezi wa timu hiyo, Said Mtanda anasema usajili uliofanyika ulizingatia mahitaji ya kiufundi na mapendekezo ya benchi la ufundi na hakuna kiongozi aliyelazimisha majina ya wachezaji wake yapitishe, hivyo anaamini wana timu bora ya kufanya vizuri.
Mtanda anasema benchi la ufundi lilipewa mamlaka yote katika usajili na litajenga timu bora ya kuleta ushindani, huku menejimenti na uongozi ukiweka mikakati ya kujenga umoja, mshikamano, nguvu ya kifedha na kuondoa majungu na vurugu ili kutoivuruga timu.
Mdau wa soka jijini Mwanza, Ladislaus Mbogo anashauri timu hiyo kuwa na watu sahihi kwenye uongozi ambao wataisaidia wataiongoza kupita njia sahihi na kufanya vizuri, kwani timu nyingi zinazopanda daraja zina kasumba na ulimbukeni wa kufumua kila kitu na kuweka watu wasio sahihi.
“Naamini wamefanya usajili sahihi ili Pamba iendelee kuwepo na watu wa Mwanza waifaidi Ligi Kuu ili msimu unaofuata ndiyo walenge kushindana na kutafuta ubingwa. Viongozi kama hawataangalia na kuendekeza majungu basi itakuwa kwaheri,†anasema Mbogo