Babati. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amewakaribisha wanafunzi wa shule mpya ya sekondari Manyara kwa kuvaa sare za shule mithili ya mwanafunzi ili kuwapa hamasa ya kusoma.
Sendiga amewakaribisha wanafunzi hao 110 mjini Babati, Manyara leo Jumatano Agosti 14, 2024 waliowasili shuleni hapo kuanza masomo yao ya kidato cha tano kwa mchepuo wa sayansi–PCM na PCB.
Akiwa na bashasha, mkuu huyo wa mkoa (RC) akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali, akiwemo Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Maryam Muhaji na Mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro Twange, alipokelewa kwa kelele za shangwe na wanafunzi hao.
Shuleni hapo, Sendiga amepokewa na mkuu wa shule hiyo, Gisela Msoffe pamoja na wanafunzi hao 110, huku wakishangilia kwa furaha kumuona mkuu huyo wa mkoa akiwa amevaa sare kama wao.
Kabla ya kufika shuleni hapo, Sendiga alitembea kwa miguu umbali wa mita 500 kutoka barabarani hadi shuleni, baada ya kushuka kwenye gari lake mkuu wa shule hiyo na wanafunzi walimkimbilia kumpokea huku wakimshangilia kwa vifijo na kupiga kelele za furaha.
Akizungumza baada ya kusalimiana nao, Sendiga amewataka wasiwe na hofu na kuongeza bidii ya kupata elimu ambayo ndiyo imewapeleka eneo hilo.
Amewaasa wasome kwa bidii na kutanguliza nidhamu kwa walimu, ili watimize ndoto na malengo yao ya baadaye katika maisha yao.
Amewashukuru na kuwapongeza wazazi waliowapeleka watoto wao katika shule hiyo mpya na kuwahakikishia watapata elimu na huduma bora, ulinzi na usalama wakati wote watakapokuwa shuleni hapo.
Hata hivyo, ameagiza umaliziaji wa miundombinu ambayo bado haijakamilika, ili ikamilike mapema na wanafunzi wapate huduma hizo hasa ya bwalo.
Awali, mkuu wa shule, Gisela Msoffe akisoma taarifa ya shule hiyo amesema ina walimu 14, tisa wa kiume na watano wa kike.
Msoffe amesema wana muuguzi mmoja, matroni wa muda mmoja, wapishi wawili wa muda na walinzi watano wa muda.
Hata hivyo, amesema wanakabiliwa na changamoto ya shule kutopokea fedha za uendeshaji, hivyo kusababisha kukosekana kwa baadhi ya huduma kama kuwalipa watumishi wasio walimu.
Amesema ukosefu huo unasababisha washindwe kununua samani za shule na kulipia gharama za chakula na shule kukosa maji ya mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Babati (Bawasa).
“Tunaishukuru Serikali kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule hii yenye miundombinu ya kisasa na mazingira bora ya ufundishaji na kujifunza,” amesema Msoffe.
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Anna John amempongeza mkuu huyo wa mkoa kwa kuvaa sare kama wao, hivyo kuwapa msukumo wa kutimiza ndoto zao.
“Mkuu wetu wa mkoa ametujengea uwezo zaidi kwa kuvaa sare kama sisi, kwani watoto wa kike tunapitia vishawishi vingi ila kwa tukio hili tumepata somo la kujifunza ili tufaulu masomo tuwe kama yeye,” amesema.
Shule ya Sekondari Wasichana Manyara ni miongoni mwa shule mpya za kidato cha tano na sita nchini za mchepuo wa sayansi zilizojengwa maalumu kupitia Serikali ya Awamu ya Sita.