Arusha. Mahakama ya Rufani imebariki adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa wakazi wawili wa Manyara, akiwemo fundi ujenzi, Mchana Mohamed, aliyehukumiwa kwa kosa la kumlawiti mtoto mwenye umri miaka miwili.
Hii ni rufaa ya pili ya Mohamed kukwaa kisiki, awali alihukumiwa kifungo hicho na Mahakama ya Wilaya ya Kiteto lakini hakuridhika, akakata rufaa Mahakama Kuu akagonga mwamba, kisha akaenda Mahakama ya Rufani, ambayo pia imeridhia hukumu ya mahakama ya awali.
Uamuzi huo umetolewa Jumanne Agosti 13, 2024 na mahakama hiyo iliyoketi Arusha chini ya jopo la majaji watatu – Dk Gerald Ndika, Abrahaman Mwampashi na Agness Mgeyekwa.
Mohamed alidaiwa kutenda kosa hilo Mei 22, 2014 katika Kijiji cha Chekanao, Kiteto mkoani Manyara.
Akitoa ushahidi mahakamani, mama wa mtoto alidai siku ya tukio alimuacha mwanawe nyumbani akiwa na kijana huyo na yeye akaenda kununua mboga na aliporejea nyumbani alikuta mlango wa nyumba umefungwa kwa ndani.
Alidai kuwa alifungua mlango huo kwa kutumia kisu na kumkuta mwanawe akilia kwa maumivu huku mtuhumiwa akiwa anapandisha suruali yake.
Anasema alipomkagua mwanawe njia ya haja kubwa alikuta ameumizwa, ndipo alitoka nje na kupiga mayowe ya kuomba msaada kwa majirani waliofika wakamkamata Mohamed na kumpeleka ya serikali ya kijiji na baadaye polisi.
Katika ushahidi wa upande wa mashtaka, Mohamed anadaiwa kukiri kutenda kosa hilo akilihusisha na shetani.
Katika utetezi wake wa kiapo, mshtakiwa huyo alikiri kuwepo eneo la tukio na kwamba alijihisi ghafla hamu ya kushiriki ngono na mtoto huyo baada ya mawazo mabaya kumuingia akilini.
Alidai kushindwa kustahimili tamaa hiyo na mwishowe alijikuta amemlawiti mtoto huyo.
Katika rufaa hiyo ya jinai namba 678/2021, Mohamed alikuwa na sababu tisa akidai kuwepo tofauti na eneo la tukio, ushahidi wa mama wa mtoto haukuwa wa kutegemewa na kuwa alikuwa na tatizo la akili.
Rufaa hiyo ilipingwa na mawakili waliomwakilisha mjibu rufaa (Jamhuri) wakisema madai ya kuwa na tatizo la akili si kweli kwa sababu wakati wa usikilizwaji wa kesi ya awali, hakuzungumzia suala hilo.
Wakili alidai wanatambua kuwa mahakama ya awali iliyosikiliza kesi hiyo ilikuwa na mamlaka ya kuchunguza afya yake ya akili, lakini mahakama hiyo iliendelea na kesi kama kawaida kutokana na Mohamed kuwa na akili timamu na uwezo wa kujitetea.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Jaji Ndika alieleza kuwa kesi hiyo ilithibitishwa bila kuacha shaka na akabariki adhabu ya kifungo cha maisha jela ambacho kimetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 154 (1) (a) cha Kanuni ya Adhabu.
Wakati hiohuo, Mahakama hiyo imebariki adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa Boay Bura, aliyekuwa anapinga hukumu ya Mahakama Kuu, iliyothibitisha kukutwa na hatia kwa kosa la ulawiti kwenye Mahakama ya Wilaya ya Babati.
Boay alishtakiwa kwa kosa la kumlawiti mtoto wa miaka saba, Januari 23, 2019 katika Kijiji cha Moyamayoka, Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara.
Uamuzi wa kesi hiyo namba 570 ya mwaka 2021 pia ulitolewa jana Agosti 13, 2024 na jopo la majaji watatu walioketi jijini Arusha – Dk Gerald Ndika, Abrahaman Mwampashi na Sam Rumanyika.
Katika ushahidi ulioungwa mkono na Mahakama Kuu na Kisha Maharaka ya rufani, ilidaiwa na upande wa mashtaka, kuwa siku ya tukio mwathirika alitumwa na mama yake kwenda kununua maziwa, akiwa njiani, Boay alimkamata na kumpeleka kwenye kichaka kilichokuwa karibu.
Ilidaiwa alimvua nguo na kumlawiti, mtoto huyo alipokuwa akilia, shahidi wa nne katika kesi hiyo ambaye alikuwa akichunga ng’ombe jirani na eneo hilo alisikia sauti akasogea karibu na kichaka akamkuta Boay akifanya kitendo hicho.
Alidai alipokuwa akimuokoa mtoto huyo, mshtakiwa alikimbia eneo hilo na yeye akampeleka mtoto huyo kwa mama yake na baadaye suala hilo likatolewa taarifa kwa Mtendaji wa Kijiji na Polisi na baadaye mtoto akapelekwa Kituo cha Afya Magara kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
Katika utetezi wake, Boay alikana kutenda kosa hilo na kudai kuwa na mgogoro wa shamba na mama wa mtoto huyo.
Mahakama hiyo ilimtia hatiani Boay na kumhukumu kifungo cha maisha jela.
Boay ambaye pia alijiwakilisha mwenyewe, alikuwa na sababu 16 za rufaa ikiwemo kuchelewa kufikishwa mahakamani, usikilizaji wa awali ulikiuka kifungu cha 192 (2) na (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kunyimwa fursa ya kuwasilisha mashahidi wake wawili.
Nyingine alidai ni shtaka na ushahidi ulitofautiana kuhusu eneo lililotokea tukio, kosa aliloshtakiwa nalo halikuthibitishwa na kudai kuhukumiwa kinyume na kifungu cha 170 cha CPA.
Katika rufaa hiyo, upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali ambaye alipinga vikali rufaa hiyo na kuomba mahakama kuitupilia mbali.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kupitia kumbukumbu za mahakama, Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali hoja zote za rufaa.
Jaji Ndika alieleza kuwa wamejiridhisha kwamba Boay alitiwa hatiani kwa kosa la ulawiti kwa mtoto wa miaka saba na adhabu hiyo ya kifungo cha maisha jela ilistahili kwake.