Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi “Sugu”, walikamatwa kwa nyakati tofauti na kuwekwa mahabusu.
Imekuwaje tena?
Hilo ndilo swali. Tanzania ambayo inaongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, mwenye falsafa ya R4; Maridhiano (Reconciliation), Ustahimilivu wenye unyumbulifu (Resilience), Mageuzi (Reform) na Ujenzi mpya wa demokrasia (Rebuilding).
Nini kimetokea? Ndani ya miaka mitatu, uongozi wa Rais Samia uliimbwa kila kona, Tanzania na nje ya taifa, kwa kujenga na kuimarisha demokrasia.
Wapinzani wake wa kisiasa walimpongeza. Walimwita Mama. Walisema ameliponya Taifa.
Mwaka 2022, Jarida la Time la Marekani, lilimtaja Rais Samia kwenye orodha ya binadamu 100 wenye ushawishi mkubwa duniani.
Time walitaja nguvu ya Rais Samia kuwa ni namna alivyoteua wanawake wengi kuongoza wizara maarufu.
Pili, jinsi Rais Samia alivyofanya mikutano na wapinzani wake, hivyo kujenga afya ya demokrasia.
“Uongozi wake umekuwa ni chachandu,” waliandika Jarida la Time na kuendelea: “Mwaka 2021 Rais Samia alifanya mabadiliko makubwa Tanzania.
“Mlango wa majadiliano ulifunguliwa kwa wapinzani wa kisiasa, hatua zimechukuliwa kujenga imani katika mfumo wa kidemokrasia, juhudi zimefanyika kuongeza uhuru wa habari na wanawake na watoto wa kike wamepata mfano wa kuiga.”
Ukiacha hoja ya kuwa wanawake na watoto wa kike kupata kiigizo chao kupitia Samia, hoja nyingine zote zilizosalia, unaweza kuziweka kwenye sentensi moja; Rais Samia amebebwa na misingi anayoiweka ya uongozi wa kidemokrasia.
Hana ubabe kwa vyombo vya habari wala wapinzani wake wa kisiasa.
Amekuwa akijishusha mpaka kwa wanaharakati ili kupata ushirikiano wa pamoja kujenga nchi; hivyo ndivyo Rais Samia alivyojijenga.
Mei 31, 2022, Rais Samia alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 30 ya Sugu kwenye muziki. Sugu ni kiongozi wa Chadema. Machi 8, 2023, Rais Samia alikuwa mgeni rasmi kwenye kongamano la Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), katika kilele cha Siku ya Wanawake Ulimwenguni.
Januari 3, 2023, Rais Samia alifuta katazo la vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara, lililokuwa limedumu kwa miaka sita. Kila mtu alifurahia. Mikutano ya hadhara ya kisiasa ikarejea. “Mama wa Demokrasia,” ndivyo baadhi ‘walivyombatiza’ jina hilo Rais Samia.
Jumatano, Januari 24, 2024, Chadema walifanya maandamano makubwa jijini Dar es Salaam. Walifanikiwa kushawishi umati mkubwa kuingia barabarani kuandamana. Mamia walisimama pembeni ya barabara na nje ya nyumba zao, kusalimia walioandamana. Mafanikio ambayo Chadema waliyapata kwenye maandamano hayo, moja kwa moja yalimjenga Rais Samia.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa chama cha upinzani Tanzania kukiri kufanya mazungumzo na Jeshi la Polisi, kisha kukubaliana kushirikiana kufanikisha maandamano ya amani. Hayo ni matunda ya aina ya siasa ambazo nchi iliingia. Siasa za kusikilizana sikio kwa sikio, badala ya kutazamana jicho kwa jicho.
Maandamano ya Chadema yalizidi kumdhihirisha Rais Samia kuwa ni mwanademokrasia mzuri, anayeamini katika uhuru wa watu kujieleza, mwenye kuridhia wapinzani wake watoe hadharani yaliyomo ndani ya vifua vyao. Zaidi alijipambanua kama kiongozi anayejiamini.
U-turn kwa tafsiri rahisi ni kugeuza ulipotoka. Kisiasa, U-turn humaanisha mabadiliko ya sera au dira. Inaitwa pia “flip-flop”.
Julai Mosi, 2022, Tanzania ilipoadhimisha miaka 30 ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, Rais Samia aliandika makala ambayo ndani yake alitambulisha falsafa ya R4. Aliahidi kuitumia ili kudumisha demokrasia nchini. Hizo R4 zipo aya ya tatu ya makala haya, pamoja na tafsiri yake.
Falsafa ya R4, iliiipa nchi pumzi mpya. Kwa miaka mitano kabla ya Samia kuwa rais, taifa lilipita kwenye tanuri lenye moto mkali wa kisiasa. Uwanja wa siasa haukuwa na usawa wala uhuru, zaidi hakukuwa na ushindani wa hoja, bali uadui na kuzibana midomo. Samia alikuja na mabadiliko makubwa.
Sanaa ya mwanasiasa mahiri, inataka awe mstahimilivu, mwenye uhusiano mzuri na wadau wenzake wa siasa, pia asikilize hoja hasi kwa uvumilivu na azielewe. Hiyo ndiyo tafsiri inayopatikana ndani ya “R4”.
Kabla ya Rais Samia, Rais madarakani alikuwa Dk John Magufuli. Enzi hizo, haikuwa ajabu kushuhudia uongozi wa juu Chadema, kwa wakati mmoja, wakiwa mahabusu. Hizi ndizo nyakati ambazo Rais Samia aliziundia falsafa ya R4 ili zisirejee.
Upo wakati, Mwenyekiti Mbowe, Katibu Mkuu, Vincent Mashinji, naibu makatibu wakuu, Mnyika (Tanzania Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar), aliyekuwa Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Peter Msigwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, Esther Matiko na wajumbe wengine wa Kamati Kuu Chadema, walishikiliwa mahabusu kwa wakati mmoja.
Wabunge wa Chadema walifungwa jela. Sugu (Mbeya Mjini) na Peter Lijualikali (Kilombero), ni mifano dhahiri. Wabunge wa upinzani kushikiliwa mahabusu, ilikuwa inakaribiana na siasa za Mashariki ya Kati, jinsi wabunge wa Palestina, ambavyo hukamatwa na kushikiliwa Israel.
Mpaka mwaka 2015 unamalizika, wabunge 12 wa Palestina walikuwa jela, wengine kwa kuhukumiwa baada ya kukutwa na hatia, wapo ambao walishikiliwa kwa nguvu za kijeshi na kuwekwa kizuizini pasipo hatua za kisheria kuchukuliwa.
Tanzania haiwezi kuwa sawa na Palestina kwa sababu wabunge wao wanakamatwa na Israel, wanashtakiwa na Israel kisha kufungwa Israel. Hata wale ambao mashtaka yao hayaendi mbele ya sheria, nao wanawekwa kizuizini na Israel.
Haikuwezekana kwa Tanzania kufikisha wabunge 12 jela kwa wakati mmoja kama Palestina, ila kuwa na mfungwa mmoja mbunge ni aibu kwa sababu yalifanyika Tanzania wakati Wapalestina wanatendewa na Waisrael.
Wabunge Khalida Jarrar, Aziz Duwaik, Marwan Barghouti, Ahmad Sa’adat, Hassan Yousef, Mohammad Jamal Al-Natsheh, Muhammad Bader, Azzam Shalhab, Nayef Rajoub, Hosni Al-Burini, Riyadh Raddad na Muhammad Abu Tir, wote hao ni wabunge wa Palestina ambao mwaka 2015 walikuwa jela kwa wakati mmoja.
Huo ulikuwa ulinganishaji kipindi cha Magufuli, kiongozi ambaye alifanya kila kitu kuhakikisha shughuli za kisiasa zinakuwa ‘haramu’.
Rais Samia, ndani ya siku 100 za kwanza ofisini, aliifanya nchi ivute hewa safi.
Haikuwa kisiasa tu, bali na maeneo mengine ambayo awali aliona yalifanyiwa ukandamizaji.
Kitendo cha uongozi wa Chadema kuwekwa mahabusu Mbeya, kinaleta tafakuri, je, kuna U-turn ya kisiasa kwa Rais Samia, kutoka kwenye falsafa yake ya R4? Vipi, U-turn hiyo inaelekeza sera za nchi mahali ambapo taifa lilitoka na ikadhaniwa isingejirudia? Zama za Magufuli na siasa za “weka ugoko niweke jiwe”.
Naikumbuka kauli ya Mbowe. Alipaza sauti, akasema “never again”, kwamba zama za Magufuli na siasa zile za kukamiana, hazikupaswa kurejea. Vipi sasa? Mambo gani ambayo yanafanya siasa za sasa zianze kushika uelekeo wa mwingine?
Kuna kijiwe kimoja, yupo mtu baada ya kunywa vikombe viwili vya kahawa alisema Rais Samia alishavumilia sana, ila uchokozi umezidi, kwa hiyo ameona bora aruhusu moto uwawakie wapinzani wake, waone kumbe naye anaweza kuwaunguza. Ni basi tu!
Jibu la mtu huyo wa kijiwe cha kahawa ni R mbili, kati ya nne za Rais Samia. Reconciliation (Mariadhiano) na Resilience (Ustahimilivu). Je, Rais Samia amechoka maridhiano au ameshindwa kustahimili? Dhahiri, nafasi bado ipo kwa Rais Samia kuketi mezani na wapinzani ili kuendeleza utamaduni aliouanzisha.
Mwingine alizungumza kwa kunong’ona, kwamba Mbowe, Lissu, Mnyika na Sugu, wamewekwa mahabusu ili kudhibiti hatari ambayo ingejitokeza. Kwamba, mkusanyiko wa vijana wa Chadema, ungechochea hisia za vijana wa kundi rika Z (Generation Z au Gen Z), kama ilivyotokea Kenya.
Mtazamo huo haujai kwenye kiganja cha hoja, maana Tanzania ina rekodi zake. Nyakati zote ambazo waandamanaji waliruhusiwa kufanya maandamano yao bila migongano na polisi, amani ilitawala na hakukuwa na tishio lolote.
Mwaka 2011, Arusha, vijana watatu walipoteza maisha, chanzo chake kilianza na udhibiti wa maandamano ya Chadema.
Baada ya mauaji hayo ya Arusha, Chadema waliandaa maandamano mengine ambayo hayakuzuiwa na polisi. Yalifanyika kwa amani, hakuna aliyeuawa wala kujeruhiwa.
Januari 26 na 27, 2001, polisi walitumia nguvu nyingi kudhibiti waandamanaji wa Chama cha Wananchi (CUF). Matokeo yake, vifo vingi vilitokea. Tanzania ilitengeneza wakimbizi ambao wengi wao walikimbilia Mombasa na Lamu, wengine walifika mpaka Somalia. Mtanzania alikimbilia Somalia kutafuta amani na usalama wa maisha yake.
Mfano mwingine dhahiri ni Januari 24, 2024, Dar es Salaam, maandamano ya Chadema ambayo yalifanyika pia mikoa ya Mwanza, Arusha na Mbeya.
Hakukuwa na shida yoyote. Amani ilitawala mwanzo mpaka mwisho. Rais Samia alicheza mpira wenye maarifa mengi ya kisiasa.
Nafasi bado ipo. Ujenzi wa demokrasia unapaswa kuwa endelevu. Kutakuwa na kujikwaa au kujisahau. Muhimu ni kutambua kwamba ulinzi wa siasa safi za nchi upo ndani ya R4.
Hivyo, inatakiwa kurejea mezani na kufanya mazungumzo, ili siku zote ipatikane hali ya kukutana katikati.
Rais Samia anapaswa kutunza taji alilovikwa la “Mama wa Demokrasia”. Nchi haipaswi kurudi ilikotoka. Zile zilikuwa zama ngumu na zilichafua taswira ya nchi.
Rais Samia tayari ameshajipambanua kiuongozi kama mpenda haki na mwanademokrasia kindakindaki. Hapaswi kupiga U-turn, ama kwa hasira au utashi.