Serikali yawaita Watanzania kuwekeza Kituo cha Biashara Ubungo, kufunguliwa Oktoba

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji wa Tanzania, Profesa Kitila Mkumbo amewaita Watanzania kuchangamkia fursa katika Kituo cha Biashara Ubungo (EACLC), jijini Dar es Salaam ambacho ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 90.

Profesa Mkumbo, amesema asilimia 95 ya maduka 2,060 yaliyopo kituoni hapo yametengwa kwa Watanzania hivyo hawana budi kuwekeza kwa ajili ya maendeleo yao pamoja na Taifa.

Hayo ameyabainisha alipopokea ujumbe wa wawekezaji kutoka Jiji la Weihai la China waliofika kituoni hapo kwa ajili ya kufungua eneo la biashara na kuwekeza.

“Faida yake katika uchumi ni kubwa kwani Watanzania zaidi ya 15,000 watapata ajira za moja kwa moja lakini pia kitalipa mwonekano mzuri jiji letu.”

Amesema ni sehemu muhimu kwa Watanzania kukuza uwezo wa kibiashara ndani, Afrika na duniani kwa ujumla.

Meneja wa Kituo hicho, Victoria Mombury amesema kitafunguliwa Oktoba 2024 kwani hadi sasa kimeshakamilika kwa asilimia kubwa.

Akizungumzia ujumbe huo kutoka Weihai amesema wanajihusisha na bidhaa za viwanda na uzoefu wa teknolojia pia huduma za usafirishaji wa bidhaa kutoka China kuja Tanzania.

Mombury amesema ugeni wa ujumbe kutoka Weihai si kwa biashara na uwekezaji pekee, bali hata ushirikiano wa kimajimbo, manispaa na Serikali kwa ujumla.

Waziri Mshauri wa ubalozi wa China Tanzania, Suo Peng amesema kituo hicho kitakua kikubwa kuwahi kutokea Afrika Mashariki na Kati ambacho kitachochea uchumi wa nchi.

Aidha, amesema EACLC itaizidi kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.

“China ipo tayari kuendelea kufanya kazi na Tanzania Ikiwemo kuagiza bidhaa nyingi za kilimo, na inaamini Serikali ya Tanzania itaendelea kuwapa ushirikiano kwa wawekezaji kutoka nchini humo na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji,” amesema Peng.

Katibu wa Kamati ya Manispaa ya CPC Weihai, Yan Jianbo, amesema Tanzania na China zina uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia ambao kwa sasa ni zaidi ya miaka 60.

“Nimefurahi  kuja kuwa mwenyeji wa kongamano la 2024 China Weihai. Sisi tumeshirikiana na Tanzania na tutaungana kwa ajili ya maendeleo ya nchi zetu hizi mbili.”

“Jengo litakuwa na ghorofa nne lenye eneo la maegesho ya magari 1,000, maduka 2,060, usafirishaji na huduma za kibenki,” amesema.

Inaelezwa kuwa kituo hicho kitakuwa cha kwanza kwa ukubwa ukanda wa Afrika Mashariki na nchi 16 za Jumuiya ya Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC), kwa kupokea wafanyabiashara.

Kwa miaka mingi China imekua mwekezaji mkubwa wa Tanzania katika miradi mikubwa ikiwa ya ujenzi. 

Related Posts