Simba, Awesu ngoma nzito, mchongo mzima uko hivi!

KAMA wewe ni shabiki wa Simba na ulikuwa unachekelea usajili wa kiungo mshambuliaji fundi kutoka KMC, Awesu Awesu pole yako, kwani dili la nyota huyo wa zamani wa Azam na Madini limebuma na jana klabu aliyokuwa akiichezea ikimtangaza kumkaribisha upya kikosini kutoka kwa Wekundu wa Msimbazi.

Awali Mwanaspoti mwishoni mwa wiki liliwajulisha kuwa dili la Awesu limewapalia Simba baada ya KMC kukimbilia Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka (TFF), kushtaki kuwa, mchezaji huyo amechukuliwa kinyemela na kupelekwa kambini, Ismailia Misri.

Mara baada ya shauri hilo kusikilizwa pamoja na lile linalowahusu Yusuf Kagoma aliyetoka Singida BS na Valentino Mashaka aliyetokea Geita Gold, Kama hiyo iliwapa ushindi KMC, licha ya taarifa iliyotolewa jana ilijaa ‘siasa’ kwa kusema wamebaini Simba haikumrubuni mchezaji, lakini ikaipa onyo kali

Katika kesi hiyo, ilitolewa maamuzi kuwa kiungo huyo arudi KMC na kama Simba inamtaka ianze upya taratibu wakati dirisha likiwa limesalia na saa chache kabla ya kufungwa usiku wa leo, kabla ya jana Wana Kino Boy kumtambulisha upya kiungo huyo kwa kumkaribisha, japo mwenewe ni kama amewanunia vile.

KMC imetaka Sh 200 Milioni ili waweze kumuachia Awesu, aliyebakiza mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo, licha ya mchezaji huyo mabosi wa klabu hiyo 50 Milioni za kuvunja mkataba huo.

Mkataba huo unaelezwa una kipengele kwamba mchezaji anaweza kuvunja na kuilipa klabu Sh 50 Milioni, lakini ikiwa na ssbabu ya msingi na hakukuwa na makubaliano ya pande mbili, zaidi ya kutambulishwa Msimbazi.

Akizungumza na Mwanaspoti Ofisa Mtendaji wa KMC, Daniel Mwakasungula alisema wamepokea maamuzi ya kamati na waliamini haki ingekuwa kwao na kwa sasa wanamsubiri Awesu ajiunge na wenzake kwa msimu mpya na iwapo kuna timu inamtaka ifuate taratibu kwani wapo tayari kumuuza.

“KMC sio klabu ndogo kama wanavyotuchukulia, klabu zingine zinatakiwa kuheshimu taratibu na kuhakikisha zinamfuata mchezaji kwa utaratibu na heshima,” alisema Mwakasungula.

Taarifa za ndani zinasema, bado klabu hiyo haijakata tamaa na mchezaji huyo.

Aidha inadaiwa, ni ngumu kwa klabu hiyo kuachana na Awesu kwani kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davids alishamuweka katika hesabu zake.

“Sio rahisi kumuacha hivyo leo (jana) na kesho (leo) tutapambana kuhakikisha tunamalizana na KMC ili kumpata kiungo huyo. Unajua hadi kocha alishampanga hadi katika dabi kabla ya kumchomoa dakika za mwishowe, hivyo kama ikimkosa kiungo huyo kazi itakuwa ngumu,” kilisema chanzo hicho kilichosisitiza lolote linaweza kutokea kabla ya dirisha kufungwa.

Licha ya Simba kutopewa msala na kamati, lakini Simba ilimtambulisha na kumpeleka kambini Awesu akiwa na mkataba wa mwaka mmoja, wakati sheria za usajili kwa mchezaji aliye chini ya miezi sita tu, klabu inayomtaka ni lazima imalizane na timu anayoitumikia tena ikiwa na nje ya ligi husika ya nchi, hivyo kuzua maswali hadi sasa kwa wadau wa soka nchini.

Inaelezwa kitendo cha KMC kumbania asiende Simba alioanza kufanya nao mazoezi Misri na hata iliporejea nchini, imemtumbukia nyongo Awesu na huenda akaikaushia mazima msimu huu kuonyesha msimamo alionao, kama alivyowahi kufanya Feisal Salum ‘Fei Toto’ alipotaka kuondoka Yanga kwenda Azam FC.

Mtu wa karibu wa Awesu aliliambia Mwanaspoti, mchezaji huyo ameweka msimamo huo, licha ya KMC, kukaribishwa tena.

“Awesu amegoma kurudi na amesema kwake hakuna kitakacho badilika kwa upande wake kwani hatarudi KMC.”

Awesu alipotafutwa kuthibitisha madai hayo hakupatikana licha ya simu kuita muda mrefu.

Related Posts