Dodoma. Kipenga cha uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2024, kitapulizwa kesho Alhamisi, Agosti 15, 2024 wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa atapotoa tangazo la uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Tamisemi, Nteghenjwa Hosseah, tangazo hilo litatolewa viwanja vya Chinangali jijini Dodoma saa 6 mchana.
“Tangazo hili litakwenda kutoa maelezo mbalimbali ya namna ya uchaguzi utakaofanyika na mtiririko mzima wa matukio ya uchaguzi wa Serikali za mitaa,” amesema Hosseah.
Miongoni mwa yatakayobainishwa ni pamoja na kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka ya miji midogo za mwaka 2024, na kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa, 2024.
Nyingine ni kanuni za uchaguzi wa Serikali za mitaa katika mamlaka ya wilaya, 2024 na kanuni za uchaguzi wa Serikali katika mamlaka za miji.
Kanuni hizo zinampa mamlaka waziri husika kutoa tangazo kwa umma kuhusu kuwapo kwa uchaguzi katika magazeti ya Kiswahili na Kingereza yanayosambazwa nchi nzima, na katika vyombo vingine vya habari si chini ya siku 90 kabla ya siku ya uchaguzi.
Pia tangazo hilo litaweka wazi ratiba ya uchaguzi na shughuli zinazohusika na masharti muhimu ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria na kanuni hizo.
Miongoni mwa mambo ambayo yamepokelewa vyema na vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla, uchaguzi huo utafanyika bila kuwepo kwa mgombea anayepita bila kupingwa kama ilivyokuwa katika chaguzi nyingine za nyuma.