UCHAGUZI WA MBUNGE WA EALA KUFANYIKA AGOSTI 27, 2024

Katibu wa Bunge anatoa Taarifa kwa Umma kwamba Uchaguzi wa Mjumbe Mmoja (1) atakayejaza nafasi wazi ya Kundi la Wanawake kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki, utafanyika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Mkutano wa Kumi na Sita unaotarajiwa kuanza tarehe 27 Agosti, 2024 Dodoma.
Pamoja na Taarifa hii, Katibu wa Bunge ambaye ndiye Msimamizi wa Uchaguzi huo, atatoa Tangazo kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa masharti yanayohusu Siku ya Uteuzi, ambayo ni tarehe 03 Septemba, 2024 saa Kumi kamili Jioni (10:00) na pia kuhusu Siku ya Uchaguzi ambayo ni tarehe 05 Septemba, 2024 saa Tano kamili Asubuhi (05:00) mara baada ya Kipindi cha Maswali.
Aidha, katika Tangazo hilo, Katibu wa Bunge atatoa Masharti yanayopaswa kuzingatiwa na wagombea wa Chama cha Siasa ambacho kina sifa ya kujaza nafasi ya Mjumbe kwa ajili ya kukiwezesha kuanza mchakato wa kuwapata wagombea kupitia Chama hicho, ambao majina yao yatawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura.
Mgombea aliyeshinda katika ngazi ya Chama anapaswa kujaza Fomu ya Uteuzi kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza na kuiwasilisha kwa Katibu wa Bunge. Fomu hiyo itatangazwa katika Gazeti la Serikali na inapatikana kwenye Tovuti ya Bunge ambayo ni www.bunge.go.tz.
Imetolewa na:- Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa,
Ofisi ya Bunge,
DODOMA.
14 Agosti, 2024.

Related Posts