Dar es Salaam. Wanamtandao wa Kupinga na Kupambana na Rushwa ya Ngono nchini Tanzania wametaka kuondolewa kwa kifungu cha 10(b) kwenye mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya rushwa, ambacho kinahukumu mtu aliyetendewa udhalilishaji huo kwa kigezo cha kushawishi.
Tamko la wanamtandao hao limetolewa leo Jumatano, Agosti 14, 2024, jijini Dar es Salaam na Mary Ndano, mjumbe wa mtandao huo, akisema kuwa kifungu hicho kitaendelea kuwalinda wanaofanya vitendo hivyo na kuwaathiri zaidi wanawake, ambao ndio waathirika wakubwa.
Ndano amesema nyongeza ya kifungu hicho ni kinyume na sheria za kimataifa, sheria za kuzuia rushwa za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika na kanuni zote zinazoongoza Muungano wa Afrika Mashariki zinazokataza rushwa ya ngono.
“Sisi wanamtandao unaopinga rushwa ya ngono, hatukubaliani kabisa na marekebisho yaliyobainishwa kwenye kifungu cha 10(b) na tunapendekeza kifutwe kabisa kwani kinakwenda kinyume na dhana nzima ya kifungu cha 25 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa,” amesema Ndano.
Ameongeza kuwa kifungu hicho kinalenga kumlinda mhalifu badala ya kuwa msingi wa kuzuia uhalifu na kulinda haki.
“Tunaviomba vyombo vyote vinavyohusika na mabadiliko ya sheria, ikiwemo Bunge, kutokubaliana na nyongeza ya kifungu hicho kwani itapelekea kuwepo kwa sheria itakayoendeleza utumiaji mbaya wa mamlaka,” ameongeza.
Hilda Dadu, mmoja wa wanamtandao, amesema kuwepo kwa kifungu hicho kutawafanya waathirika kuogopa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanapofanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, ikiwemo rushwa ya ngono.
“Jambo hilo linaweza kuchochea kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii, ambapo waathirika wakubwa ni wanawake na watoto,” amesema Dadu.
Ametoa wito kwa wanaume nao kuungana pamoja na wanawake kupinga kupitishwa kwa kipengele hicho kwani kinaweza kupelekea kurudi nyuma kwa mapambano dhidi ya rushwa ya ngono.
Rose Marandu amesema jamii inapaswa kuungana kukemea vitendo hivyo kwani vinaathari katika ustawi wa uchumi na jamii kwa ujumla, hasa kwa waathirika.
Amesema vitendo hivyo vinaathiri kwa kiwango kikubwa uchumi wa Taifa kwa kusababisha matumizi mabaya ya rasilimali watu, hivyo kudhoofisha jitihada za kupambana na umaskini.
“Vitendo hivi vinahujumu utu wa Taifa kwa kugeuza haki kuwa upendeleo kinyume na maadili ya utendaji kazi na kinyume na mikataba na makubaliano ya kimataifa na kikanda yanayokataza vitendo vya rushwa ya ngono,” amesema Marandu.
Ameongeza kuwa vitendo hivyo humpokonya na kumdhalilisha mtu utu wake, kumnyima fursa za kukuza vipaji vyake, na kumfanya kuwa mtumwa wa ngono, huku zikitolewa nafasi za upendeleo kwa asiye na sifa stahiki.