HATIMAYE George Mpole amerejea nyumbani baada ya kucheza kwa misimu miwili ugenini huko DR Congo.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Geita Gold, amejiunga na Pamba ya Mwanza ambayo imenasa saini yake akitokea FC Lupopo ambayo alijiunga nayo mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2021/2022.
Suala la George Mpole kushindwa kudumu na kung’aa katika Ligi ya DR Congo lilikuwa wazi na kilichokuwa kinasubiriwa ni kuona kama atarudi nyumbani au atatafuta malisho kwingine.
Aliondoka Tanzania akiwa staa baada ya kuongoza kupachika mabao katika Ligi Kuu lakini mambo hayakuwa kama yalivyotegemewa kule DR Congo ambapo alitazamwa kama mchezaji wa kawaida.
Hiki kilikuwa kipimo cha ukomavu kwa Mpole na ndio kinatengeneza utofauti wa wachezaji katika harakati za kutimiza ndoto zao lakini mtihani huu ulionekana kuwa mgumu kwake ambapo dalili za kukata tamaa zilianza kujitokeza mapema.
Nyakati fulani aliiingia katika mgogoro na timu hiyo na kujikuta akitumia baadhi ya nyakati akiwa Tanzania badala ya DR Congo ambako kituo chake cha kazi kilikuwepo.
Bahati mbaya nyingine ya Mpole ni Ligi ambayo aliamua kukimbilia kutokuwa na mvuto mkubwa kama hii ya Tanzania Bara aliyoiacha hivyo hata vile ambavyo alikuwa anafanya huko vikawa havifuatiliwi au kuwa mjadala.
Kutoka kuonekana moja kwa moja kila wikiendi katika Kamera za Azam Tv hadi kucheza katika ligi ambayo haionyeshwi wala taarifa zake haziripotiwi kwa kiasi kikubwa ni wazi kwamba Mpole alikuwa amejirudisha nyuma kwa kuamua kwenda Lupopo.
Mwisho wa siku kuanza moja sio vibaya kama ukigundua umekosea hivyo tunamkaribisha Mpole nyumbani aanze kujitafuta upya.