Ni mgahawa uliopo jirani na kituo cha mwendokasi cha Gerezani, Kariakoo ambapo watu wanapata chakula na wengine wanakunywa vinywaji.
Pembezoni mwa mgahawa kuna lango la kuingia chini ya ghorofa hilo ambako watu wanaingia na kutoka. Maiko, kijana aliyevalia nadhifu anachomoka kutoka katika shimo hilo na kutokeza kwenye mgahawa, anakaa kwenye kiti huku mikono yake ikifunika paji la uso.
Anaonekana kuchanganyikiwa. Muda mfupi anatoka Lumuli kutoka shimoni humo na kukaa jirani na Maiko. Umefanya nini kaka? Kwa nini hukunisikia pale uliposhinda tuondoke? Anauliza Lumuli mfululizo. Daaa! We acha tu! Yaani hapa hata sielewi. Mzigo umeshaandaliwa China, tutalipia nini? Anaongea Maiko kwa hasira.
Wanatulia kwa muda huku watu wa pembeni yao wanafuatilia maongezi yao. Lengo ni kufahamu ameliwa kiasi gani leo. Yaani dakika kumi tu milioni hamsini imekwenda! Nitawaambia nini wateja? Anaendelea kuuliza Maiko. Sikiliza kaka, wateja hao ni kitu kidogo, umefikiria kuhusu tutalipaje mkopo wa benki? Akauliza Lumuli huku akimkazia macho.
Maiko akainuka kama mtu aliyezinduka usingizini. Akamtazama Lumuli na kuvua kofia yake. Milioni 150 na hatuna mzigo wowote wa kuuza kupata pesa hiyo, Mungu wangu! Akang’aka Maiko. Unafikiri tufanye nini? Akauliza Maiko huku anamgeukia Lumuli. Hali hii ni mbaya sana, sioni jinsi tutakavyoweza kuvuka hii changamoto! Akajibu Lumuli.
Mbona kama unaniachia peke yangu? Fikiria suluhisho kaka! Analalamika Maiko. Suluhisho lipi hapa? Wateja waliolipia mzigo wapo ofisini, watu wa benki wanahitaji rejesho baada ya siku tatu, unafikiri tutafanya nini? Anaeleza Lumuli kwa kuuliza. Daa! Kamari sio nzuri kaka. Ninaona kabisa tunakimbia mji! Anaendelea Lumuli.
Tunakimbiaje mji? Tunaondokaje bila kurejesha pesa zetu tulizoliwa kwa muda mrefu? Anauliza Maiko huku anasimama na kumsogelea Lumuli. Utarejesha kwa kutumia hela ipi? Anauliza Lumuli. Tunahitaji kuazima pesa ili tuje tucheze tena ili tukomboe pesa zetu.
Haiwezekani kukata tamaa kirahisi! Anasisitiza Maiko. Utaazima kwa nani? Watu wote umeshawaazima na hujawarejeshea. Zamani ulikuwa unaazima kwa ajili ya kuagiza mzigo, lakini kwa sasa kila mtu anajua kuwa unaazima ili kucheza kamari. Anaeleza Lumuli.
Lakini watu walisema kamari inatajirisha, mbona kwetu inakuwa kinyume? Anauliza Maiko. Sio kwamba iko kinyume, unakumbuka yule mtaalamu aliyetupa kitabu kuhusu saikolojia ya michezo ya kubahatisha? Anauliza Lumuli. Hapana sikumbuki. Anajibu Maiko kwa kifupi. Yule jamaa alisema kamari inatajirisha, lakini ni kwa upande wa mchezeshaji na sio mchezaji. Kachukue kitabu kile na ukisome tena. Akamaliza Lumuli.