*Abainisha mikakati ya serikali vijana kujiajiri na kuajiri.
*Asema Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana kuzinduliwa.
Na. Mwandishi wetu – Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema serikali imedhamiria kuendelea kutekeleza programu za uwezeshaji vijana wenye vipaji vya na wajasiriamali ili kuweza kuanzisha na kuendeleza miradi na ubunifu wao pamoja na ujuzi wao ili waweze kujiajiri na kuajiri vijana wenzao.
Mhe. Ridhiwani amebainisha kuwa tayari mikopo kupitia baadhi ya Halmashauri imeanza kutolewa. Aidha amefafanua kuwa ufanisi wa uratibu wa shughuli za Uwezeshaji vijana nchini utasimamiwa kikamilifu ili vijana waweze kunufaika na fursa za kiuchumi nchini. Ameyasema hayo leo Julai 31, 2024 Jijini Dodoma wakati akifunga kongamano la vijana kuhusu ushiriki wa vijana katika uongozi na utawala na mageuzi ya kiteknolojia kwa maendeleo ya kiuchumi.
Aidha, Waziri Ridhiwani amesema Serikali tayari imetunga Sheria ya Baraza la Vijana la Tanzania Sura Namba 441 na Kanuni zake ili kufanyia kazi changamoto za vijana na kupata chombo bora cha kuishauri Serikali katika Masuala ya Maendeleo ya Vijana nchini.
“Jitihada za Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa vijana wanajengewa uwezo ili wawezesha kujiajiri na kuajiri vijana wenzao na hivyo kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi wa nchi yetu.
Awali akizungumza Mkurugenzi wa DOYODO, Rajabu Nh’unga ameiomba serikali kuendelea kuwajengea mazingira wezeshi vijana ili waweze kijiajiri na kuajiriwa.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya kiserikali Bi. Mwantumu Mahiza ameishauri serikali kuwa na makongamano kuanzia ngazi ya wilaya ili vijana waweze kufikiwa katika kila Mkoa nchini na hatimaye kushiriki kikamilifu kutatua changamoto zao.