Mwelekeo mpya uchaguzi wa Serikali za mitaa

Dodoma. Katika hatua inayoashiria mwelekeo mpya wa demokrasia nchini, Serikali imetangaza kanuni mpya za uchaguzi wa Serikali za mitaa, ambazo zinatoa mwanya wa mabadiliko makubwa katika mchakato wa uchaguzi.

Moja ya mabadiliko makubwa ni kuondolewa kwa utaratibu wa wagombea kupita bila kupingwa, jambo lililokuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu na vyama vya upinzani.

Leo Alhamisi Agosti 15, 2024, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ametoa tangazo la uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Tofauti na uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24, 2019 ambapo vyama vya upinzani vya Chadema, ACT –Wazalendo, CUF, UMD, CCK, NCCR-Mageuzi, NLD na Chauma vilitangaza kujitoa kwenye uchaguzi huo na wagombea wengi wa CCM kupita bila kupingwa, mwaka huu hakuna kupita bila kupingwa.

“Utaratibu wa uteuzi wa mgombea pekee: Endapo kutakuwa na mgombea mmoja halali wa nafasi ya uenyekiti wa kijiji, kitongoji, ujumbe wa halmashauri ya kijiji, uenyekiti wa mtaa au ujumbe wa kamati ya mtaa, Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi atamteua mwombaji huyo kuwa mgombea pekee kwa nafasi aliyoomba,” amesema Mchengerwa.

Mwaka huu hali itakuwa tofauti, kwani wagombea wote watahitaji kupigiwa kura za “Ndiyo” au “Hapana,” hata kama ni wagombea pekee wa nafasi husika.

Mchengerwa ameeleza kwamba uteuzi wa wagombea utafanyika siku 19 kabla ya uchaguzi, wagombea watakaojitokeza pekee watapigiwa kura ili kuthibitisha au kukataliwa na wananchi.

Katika tangazolake, Waziri Mchengerwa ameeleza masharti muhimu yanayoongoza uchaguzi huo, akibainisha nafasi zinazogombewa ni pamoja na mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri za vijiji (kundi la mchanganyiko na la wanawake pekee), na wenyeviti wa vitongoji. Uchaguzi utafanyika kwa kufuata kanuni maalumu zilizotangazwa na Serikali.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, uandikishaji wa wapiga kura utafanyika siku 47 kabla ya uchaguzi, na utaendeshwa kwa muda wa siku 10 katika majengo ya umma.

Msimamizi wa uchaguzi atahakikisha mipaka ya vitongoji na vijiji imetangazwa siku 72 kabla ya uchaguzi ili kuruhusu wananchi kujiandikisha na kupiga kura katika maeneo yao.

Mchengerwa amefafanua kuwa, mgombea au mtu aliyeomba kuteuliwa anaweza kuweka pingamizi kuhusu uteuzi wa wagombea ndani ya siku mbili baada ya uteuzi kufanyika.

Pingamizi hilo litasikilizwa na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, na uamuzi utatolewa ndani ya siku mbili. Aidha, kutakuwa na Kamati ya Rufaa katika kila wilaya kusikiliza pingamizi hizo.

Akizungumzia taratibu za upigaji kura, Mchengerwa amesema kwa mujibu wa kanuni, kura zitapigwa kwa usiri.

Mchengerwa amesema waangalizi wa ndani wataruhusiwa kushuhudia mchakato wa uchaguzi baada ya kupata kibali maalumu kutoka kwa katibu mkuu wa wizara inayohusika.

Amesema kampeni za uchaguzi zitaanza siku saba kabla ya siku ya uchaguzi na vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi vitatakiwa kuwasilisha ratiba ya mikutano yao kwa Msimamizi wa Uchaguzi kabla ya kuanza kampeni hizo.

Serikali za mitaa zimepewa mamlaka muhimu chini ya Ibara ya 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ibara hii inaeleza wazi kuwa Serikali hizi ni vyombo vya haki vilivyoundwa ili kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika mipango na utekelezaji wa shughuli za maendeleo pamoja na utoaji wa huduma katika maeneo yao, lengo likiwa ni kuchochea maendeleo ya jamii na ustawi wa wananchi.

Uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mitaa unachukuliwa kuwa ni matakwa ya kikatiba na kipimo cha demokrasia, ambapo wananchi wote wanapata fursa sawa ya kushiriki katika maamuzi ya kitaifa kuhusu masuala ya umma.

Hii ni sehemu muhimu ya mfumo wa kidemokrasia nchini, ikiwakilisha sauti ya wananchi katika ngazi za chini za utawala.

Kwa mujibu wa Ibara ya 146(2) ya Katiba, Serikali za mitaa zimepewa majukumu kadhaa muhimu. Kwanza, zinawajibika kutekeleza kazi za Serikali kuu ndani ya eneo lake, ikiwemo kuhakikisha utekelezaji wa sheria na kuimarisha ulinzi wa wananchi.

Hili linahusisha kuhakikisha kwamba haki na usalama wa wananchi vinalindwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Pili, Serikali za mitaa zinapaswa kuimarisha demokrasia katika maeneo yao.

Hii inamaanisha kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika maamuzi yanayowahusu, hasa kupitia michakato ya uchaguzi na majukwaa ya mijadala ya umma.

Katika mazingira haya ya kidemokrasia, Serikali za mitaa zinachangia kuharakisha maendeleo kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki moja kwa moja katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.

Hivyo, utekelezaji wa majukumu haya ni muhimu katika kuimarisha utawala bora, uwajibikaji, na demokrasia ya kweli katika ngazi za chini za utawala, na hatimaye kuchochea maendeleo endelevu kwa wananchi.

Related Posts