Mwili wa mtoto wakutwa kwenye pagala baada ya kuuawa kikatili

Dar es Salaam. Ukatili kwa watoto umetamalaki! Ndiyo neno unaloweza kusema baada ya mwili wa mtoto Nashfat Abimu (6), kukutwa kwenye pagala lililopo Mtaa wa Jeshi la Wokovu na Kizuiani, Mbagala akidaiwa kuuawa kikatili.

Tukio hili limeacha simanzi kwa familia na jamii nzima, huku wengi wakitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na mauaji hayo ya kikatili.

Alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amekiri kupata taarifa ya tukio hilo, akieleza uchunguzi wa awali unaonyesha alibakwa na wakati akifanyiwa kitendo hicho alikuwa amezibwa mdomo.

“Mazingira ya mwili uliokuwa kwenye pagale eneo la bondeni karibu na Mto Mzinga tumeukuta na kitambaa mdomoni, mwili hauna jeraha lingine lolote zaidi ya dalili za kubakwa na kupotezwa maisha,” amesema.

Kamanda Muliro amesema taarifa zinaeleza mtoto huyo alikuwa ametoka shuleni na baada ya kufika nyumbani alipewa chakula, na alitakiwa akimaliza kula aoshe vyombo.

“Alikaidi kufanya hivyo akaondoka kwenda kucheza, hakurejea nyumbani kulingana na mazingira yaliyotokea kwa kuhofia kupigwa lakini baadaye alikutwa amebakwa kwenye jengo ambalo halijamalizwa kujengwa na amepoteza maisha leo (jana) asubuhi Agosti 14, 2024” amesema.

Kamanda Muliro amesema kwa kuwa kitendo hicho ni kosa la jinai, Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watuhumiwa na kukusanya ushahidi wa kutosha ili watakaobainika kuhusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

“Tumekuwa tukipambana na makosa haya ya ukatili wa watoto, tumekuwa tukipita maeneo mbalimbali na maeneo korofi kwa kuzingatia takwimu ni Mbagala Kuu, Mbagala Chini na Kibonde Maji kutoa elimu ya kupinga ukatili,” amesema.

Akisimulia tukio hilo lililotokea Agosti 14, 2024, Ashura Said mkazi Mbagala, Mtaa wa Jeshi la Wokovu, wilayani Temeke, amesema akiwa kwenye biashara zake nyumbani kwake saa tano asubuhi, ghafla aliwasikia watoto wakipita na kusema kuna mtoto kafa.

“Niliposikia watoto wanasema kuna maiti ya mtoto niliwaita na kuwauliza nini kimetokea wakaniambia kuna mtoto kafa kwenye jumba bovu, ndipo nilipokusanya wenzangu kwenda kushuhudia,” amesema. Amesema walipofika katika jumba hilo waliangalia hawakuona mtu yeyote akisema walijiona wajinga kwa kudanganywa na watoto.

Amesema mmoja wao aliwaeleza watoto siyo wajinga, hivyo warudi kupekua chumba kimoja hadi kingine.

“Mara ya kwanza hatukupita vyumba vyote hivyo haikuwa rahisi kugundua kama kweli kuna mtoto amefariki, hadi tulipofanya ukaguzi wa chumba kimoja kimoja ndipo tulimkuta mtoto kwenye chumba kidogo (choo cha ndani) akiwa wazi na sehemu zake za siri zikiwa kama zimetolewa,” amesimulia Ashura.

Amesema alitumia kitenge chake kufunika mwili wa marehemu, kisha wakawaita watu wengine na kumpiga simu Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Jeshi la Wokovu, Chauka Kikwesha.

Mwenyekiti huyo amesema, “niliposikia vile imebidi nikusanye watu wangu akiwepo mtendaji tukaenda kwenye tukio baada ya kuona kilichopo niliwapigia simu viongozi, akiwamo diwani na polisi kata na wao walitoa maelekezo ya watu kutokugusa mwili hadi Polisi wafike,” amesema.

Kikwesha amesema walifika askari Polisi kutoka Kituo cha Maturubai.

“Tukio hili kwetu ni la kwanza na huyu mtoto hakai mtaa huu tumesikia anaishi Kizuiani,” amesema.

Kikwesha amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi kuwalinda watoto kutokana na matukio wanayoyasikia, na wamekuwa wakipita katika mashina ya mtaa wao kuzungumza na wananchi.

Akizungumza na Mwananchi akiwa nyumbani kwake, baba mzazi wa mtoto huyo, Abimu Hassan amesema Agosti 12, 2024 alipigiwa simu na mke wake akiwa kazini mkoani Tanga.

Amesema alipewa taarifa kuwa mtoto haonekani hivyo aliomba ruhusa na kupatiwa siku saba kwa ajili ya kuja Dar es Salaam kumtafuta binti yake, kutokana na ugeni katika mtaa huo ambao wamehamia miezi miwili iliyopita.

“Jumatatu aliandaliwa na mama yake kwa ajili ya kwenda shule kwani anasoma Shule ya Msingi Mbagala na alimpeleka hadi shule akitarajia kumfuata saa tano, maana mtoto wangu alikuwa anasoma darasa la kwanza,” amesema.

Amesema ilipofika saa tano mama yake akitaka kutoka alishangaa kumuona mtoto akiwa amerudi mwenyewe, hivyo alimkanya asirudie kufanya hivyo hadi atakapokwenda kumchukua hata kama rafiki zake watamwambia warudi.

“Baada ya kumsema alimpa chakula yeye na wadogo zake ambao ni pacha na alipomaliza alitoka na ndugu zake kucheza kibarazani, wakati huo wamegawana yeye alicheza na Hassan na Hussein akicheza na wengine,” amesema.

Abimu amesema kwa kuwa mtoto wake hakuwa na utaratibu wa kuzurura alimuagiza mdogo wake juba ili aende chuo na alipopewa wakiwa wamekaa wanacheza, ghafla Nashfat alikimbia na haikujulikana anaenda wapi.

Amesema kwa kuwa aliomba juba mama yake alimuita ili ampeleke chuo lakini hakuitikia.

Amesema alipotoka nje kuuliza alipokwenda mdogo wake Hassan Abimu (2) alionyesha kwa kidole alipoelekea dada yake na mama yake alifuata njia alioonyeshwa.

“Alielekea njia ambayo aliambiwa huku akiuliza baadhi ya watu akiwepo fundi seremala ambaye alimjibu amemuona amepita na kufikiri mama yake amemtuma dukani, lakini haikuwa hivyo,” amesema.

Amesema baada ya kumkosa alirudi nyumbani na kuomba majirani wamsaidie kumtafuta muda huo ukiwa saa 8.00 mchana.

Wakati wakiendelea kumtafuta amesema ulitolewa ushauri wa kwenda kutoa taarifa msikitini, Serikali ya mtaa wa Mbagala na Kituo cha Polisi Maturubai, huku wakiendelea kusambaza picha yake katika maeneo tofauti ya Mbagala.

Amesema alfajiri ya jana baada ya kutoka msikitini aliamua kwenda kumtafuta mtoto na ilipofika saa tisa alipigiwa simu na ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mbagala akaambiwa mtoto amepatikana Kichemchem anatakiwa kwenda huko.

“Nilifika kwenye tukio nilikuta askari nilipoonyeshwa mwili kabla ya kufunua nilipoona gauni nilijua ni mtoto wangu na nilipofunuliwa usoni namuona mwanangu Nashfat sikuamini kama ni wangu nilitamani iwe ndoto kwa nilichokiona,” amesema.

Amesema hakuwa na nguvu maana amewaza vitu vingi kwani mtoto wake hakuwa na tabia ya kutoka, na alikuwa mtoto mtiifu kwa kila mtu na hajui ni nini kilitokea hadi akakimbia ghafla na kukutwa na mauti.

Amesema mwili ulipelekwa katika Hospitali ya Polisi Kilwa Road kwa ajili ya uchunguzi.

Mtoto huyo amezikwa leo Agosti 15, 2024 katika makaburi ya Kizuiani.

Related Posts