Wananchi Afrika Mashariki na hisia zao kuhusu uchumi wa nchi zao

Dar es Salaam. Asilimia 69 ya Watanzania wanaridhishwa na mwelekeo wa Serikali yao, Wakenya ni asilimia 42 na Waganda ni asilimia 51, Ripoti ya Sauti za Wananchi iliyotolewa na Taasisi ya Twaweza imeeleza.

Ripoti hiyo ni matokeo ya utafiti uliofanywa kuanzia mwaka 2013 katika mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda, ukihusisha watu 4,483, ambao 1,520 ni kutoka Tanzania (mikoa ya Kigoma na Dar es Salaam), 840 kutoka Kenya (Kaunti ya Makueni) na 2,123 kutoka Uganda (Kampala, Kyotera na Tororo).

Ripoti hiyo, maarufu kama ‘Sauti za Watu’ inatumia zaidi njia ya simu katika tafiti zake, walengwa ni wale walio na umri wa kuanzia miaka 18 na zaidi. Jumla ya saa 74,000 zilitumika katika mahojiano hayo.

Kwa mujibu wa utafiti huo, idadi ya walioonyesha mwelekeo mbaya wa Tanzania imeizidi ile ya mwaka 2021 ambao walikuwa asilimia 16, huku asilimia 18, wakiona inaelekea pazuri.

Kati ya asilimia 25 (robo ya waliohojiwa) wanaoonyesha nchi ipo katika mwelekeo mbaya, asilimia 26 ni wanawake na wanaume ni asilimia 24.

Kundi lingine ambalo ni asilimia 44 linaonyesha halijui chochote kuhusu mwelekeo wa nchi kwa mwaka 2022.

Kundi lisilojua chochote kuhusu mwelekeo wa Taifa, lilijitokeza pia mwaka 2021, ambalo ni asilimia 66.

Utafiti huo unaonyesha mwaka 2012/14, asilimia 73 ya wananchi waliona Taifa lina mwelekeo mbaya.

“Kati ya mwaka 2017 na mapema 2021, Watanzania wengi waliona nchi inaelekea pazuri na tangu mwaka 2021, wananchi walionyesha kupunguza imani zao na wengi hawakujua kama ilielekea pazuri au pabaya.”

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Tanzania, Kenya na Uganda ripoti inaonyesha asilimia 52 waliona mwelekeo mbaya wa Taifa la Kenya, huku asilimia 48 waliona hivyo kwa Uganda mwaka 2022.

Sambamba na mitazamo hiyo ya wananchi juu ya mwelekeo wa mataifa hayo, ripoti hiyo imeweka bayana mambo yanayowaathiri wananchi kiuchumi, kijamii na kiuongozi. Wananchi katika mataifa yote wanalia na ugumu wa maisha.

Kwa upande wa uchumi, Watanzania wanaathiriwa zaidi na gharama za maisha, umasikini, ukosefu wa ajira, njaa, ardhi na kilimo kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Kenya na Uganda wao wanaumizwa zaidi na mfumuko wa bei, ukosefu wa chakula, kukosekana kwa ajira na tabaka kubwa kati ya wenye nacho na wasionacho.

Kwa upande wa huduma za kijamii, wananchi wa mataifa hayo matatu wote wanaathiriwa zaidi na huduma za afya, usafirishaji, miundombinu (isipokuwa Kenya), elimu bora na upatikanaji wa maji safi.

Wakati athari za kiuchumi na huduma za jamii zikigusa maeneo hayo, ripoti inataja rushwa, usalama wa watu kama changamoto kubwa, kwa Kenya linaongezeka moja la uongozi mbovu.

Ripoti hiyo pia imeeleza asilimia 42 ya Watanzania waliohojiwa wamesema vipato vyao vinakidhi mahitaji yao ya siku kwa Oktoba, mwaka 2020.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, asilimia 67 ya Watanzania waliohojiwa hawaelewi kuhusu hali zao za maisha, huku asilimia 20 wakisema ni mbaya, na asilimia 13 wakiona nzuri zaidi.

Shughuli za kilimo zimetajwa na ripoti hiyo kuwa ndiyo chanzo kikuu cha mapato cha kaya za Tanzania, zikitegemea kwa asilimia 39, ikifuatiwa na kujiajiri asilimia 38, kisha ajira rasmi asilimia 10, kazi za kawaida asilimia saba na mafao ya kustaafu ni asilimia nne.

Hali hiyo ni tofauti na Uganda, ambayo kwa sehemu kubwa kaya zinategemea kazi za kawaida kama chanzo kikuu cha mapato kwa asilimia 37, huku kilimo kikitegemewa kwa asilimia 25 pekee na Uganda kaya zinategemea zaidi kilimo kwa asilimia 69.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 73 ya Watanzania wana mtazamo chanya zaidi kuhusu mazingira wezeshi ya biashara nchini kwao kuliko Waganda (63), huku Wakenya asilimia 45 wakiwa na mtazamo hasi zaidi kuliko wote.

Watu wanne kati ya kumi (asilimia 41-44) nchini Kenya wana akaunti ya benki, idadi ambayo ni kubwa zaidi ikilinganishwa na Tanzania (asilimia 17-19) na Uganda (asilimia 8). Katika nchi zote tatu, wanaume wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na akaunti ya benki kuliko wanawake na pia wana uwezekano mkubwa wa kuwa na akaunti ya pesa za simu.

Hata hivyo, katika nchi zote tatu, ujumuishaji wa kifedha unasukumwa zaidi na huduma za pesa za simu, ambazo zimewezesha fursa salama na za gharama nafuu kwa wananchi katika kanda hii kupata faida za benki – uhamisho wa fedha, akiba, mikopo na matumizi bila pesa taslimu.

Kwa upande wa hali ya kiuchumi, Watanzania asilimia 50 waliohojiwa wameeleza hawaelewi kuhusu uhalisia wao wa kiuchumi, asilimia 14 wamesema ni mbaya, na asilimia 16 wakisema nzuri zaidi.

Katika mwaka 2020, asilimia 36 wamesema wanaridhishwa na mwelekeo wa Serikali katika kutengeneza kipato na fursa za ajira, huku asilimia 28 wakisema hawaridhiki, na asilimia 37 hawajui.

Kuhusu kupunguza gharama za maisha, asilimia 49 wanaridhishwa, asilimia 17 hawaridhishwi, huku asilimia 35 wakiwa hawaelewi.

Asilimia 41 ya Watanzania waliohojiwa, wamesema wanamiliki biashara kwa sasa, huku asilimia 47 hawakuwahi kumiliki, na 12 walimiliki lakini hazikudumu.

Ripoti inaonyesha mwaka 2020, Watanzania kwa asilimia 40 walikuwa na hofu ya kuishiwa na chakula, huku asilimia 20 walikuwa na njaa lakini walishindwa kula, na zaidi ya asilimia 10 walishinda na njaa kutwa.

Kwa mujibu wa utafiti huo, Watanzania waliohojiwa wanamiliki zaidi ardhi (kwa asilimia 77), kuliko vyombo vya usafiri ambavyo pikipiki ni kwa asilimia 12, gari asilimia mbili, baiskeli asilimia 46, huku asilimia 34 ya waliohojiwa wakilimiliki mifugo.

Mbali na hilo, waliohojiwa wamesema wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji ya kunywa.

“Kwa wastani Watanzania wanatumia dakika 49 kutafuta maji ya kunywa kwa maeneo ya mijini,” inaeleza sehemu ya ripoti.

Hata hivyo, njia mbalimbali ndizo zilizotajwa kutumika zaidi kuyatibu maji hayo ya kunywa kwa asilimia 62 Tanzania, huku asilimia 50 wakichemsha na asilimia tisa wakiyachuja kwa nguo.

Ripoti inaeleza asilimia tano hutibu maji kwa kemikali, asilimia moja wanayaacha yatulie ndipo yatumike, asilimia moja wanayachuja kwa chujio la maji, na asilimia 0.1 hutumia njia nyinginezo.

Kwa asilimia 28 Watanzania waliohojiwa wanaishi mbali na vituo yanapopatikana maji, asilimia 23 wanakabiliwa na uhaba wa vituo hivyo, asilimia 20 maji machafu, na asilimia 21 ni usambazaji mbaya wa huduma hiyo.

Ripoti pia inaeleza asilimia 10 ya Watanzania wameripoti kukumbwa na gharama kubwa za maji, asilimia nane wanajua vilipo vituo vya maji lakini havifanyi kazi, na asilimia 23 hawana tatizo la maji.

Wananchi wa nchi zote tatu wanajivunia uraia wao, ingawa Wakenya wana uwezekano mdogo wa kujitambulisha kwanza kama raia, Tanzania ni asilimia 63, Kenya asilimia 26 na Uganda asilimia 52%.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mchambuzi wa Masuala ya Kijamii aliyezungumza akiwa nchini Kenya, Charles Obbo amesema kilimo ndiyo shughuli kuu nchini Kenya, lakini inashangaza chanzo kikuu cha mapato ya wananchi ni shughuli za kawaida.

“Kenya inafahamika kilimo ndiyo uti wa mgongo na nilitegemea tungekuwa tegemeo kwenye eneo hilo, lakini wananchi wanategemea shughuli za kawaida kupata kipato, hii ni kutokana na yanayoendelea kwenye jamii ambayo yanawaondoa watu kulima na kutegemea vitu vingine,” amesema.

Mtafiti wa Masuala ya Kijamii kutoka Kenya, Christine Mwangi amesema jambo lililomshangaza kupitia takwimu hizo ni kuona imani ya wananchi ikipungua kwenye matumizi ya vituo vya huduma za afya vinavyomilikiwa na Serikali.

“Pia nimebaini namna ambavyo usalama wa chakula nchini Kenya upo chini na watu hawana imani na huduma za kijamii kutokana na kupoteza imani dhidi ya Serikali na watawala, watu wanajiuliza kama huduma hawawezi kuzifikia wala kuzipata kwa nini viongozi waliopo waendelee kuwepo,” amesema.

Amesema ni muhimu Serikali ione namna gani inazitumia takwimu hizo kutatua matatizo yaliyopo.

“Nchini Kenya asilimia 75 ya wananchi hawana kipato cha kupata mlo wao wa kila siku,” amesema.

Mwanahabari kutoka Tanzania, Sammy Awami amesema ukosefu wa ajira ndiyo changamoto kubwa nchini, ndiyo maana kila unapokwenda utakutana na watu wakiuza bidhaa mbalimbali barabarani.

“Ukienda maeneo mbalimbali barabarani utakutana na watu wakiuza vitu na hii ni kutokana na kukosekana kwa ajira rasmi, hivyo watu kuamua kuingia kwenye ujasiriamali,” amesema.

Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Timoth Lyanga, aliimbia Mwananchi kuwa kila ongezeko linaloshuhudiwa kwa Tanzania linatokana na maboresho ya kisera yanayofanywa na Serikali.

Amesema kazi imefanyika kuhakikisha maisha ya watu yanaimarika kiuchumi na kijamii, ingawa zipo changamoto zinazowakabili.

Amesema mwelekeo mbaya wa Taifa unategemea na eneo linalohusishwa, lakini kiuhalisia kuna matumaini. “Tukiangalia hatuwezi kusema ni mwelekeo mbaya kwa sababu hakuna vitu vilivyotajwa kuhusu mwelekeo huo,” amesema.

Related Posts