Watatu wafariki malori mawili yakigongana, kuteketea Kahama

Mwanza. Watu watatu ambao majina yao hayajatambulika wamefariki dunia papo hapo, huku mmoja akijeruhiwa kwa kukatika miguu katika ajali iliyohusisha malori mawili.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi ajali hiyo imetokea leo Alhamisi Agosti 15,2024 saa 5:30 asubuhi eneo la Manzese mjini Kahama mkoani Shinyanga.

Kamanda Magomi amesema ajali hiyo imehusisha magari mawili likiwemo lori lenye shehena ya kahawa lililokuwa likitokea Bukoba mkoani Kagera kwenda uelekeo wa Dar es Salaam kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa limebeba juisi likitokea Dar es Salaam kwenda Runzewe mkoani Geita.

“Lori lililokuwa limebeba kahawa, lilikuwa linaendeshwa na Omary Haji katika gari hilo kulikuwemo watu wawili ambao miili yao imeteketea kabisa na bado hawajatambuliwa. Lingine lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Runzewe lilikuwa limebeba Juisi na linaendeshwa na Rajab Tabu ambaye ni utingo.”

“Khalfani Mikidadi alikuwa dereva wa lori la juisi yuko chumba cha upasuaji na amekatika miguu yote miwili, mwingine ni abiria anaitwa Adam haongei kabisa. Kwa maelezo ya utingo, gari hilo lilipofika Manzese aliona gari la mchanga mbele yake limesimama ghafla akatanua kushoto zaidi ya barabara, ndipo akakutana na lori lililobeba kahawa kutoka Bukoba na kugongana uso kwa uso na kuwaka moto,” amesema Magomi.

Kamanda huyo amewataka madereva wa vyombo vya moto kufuata sheria na kanuni wanapokuwa barabarani, huku akionya Jeshi hilo halitomfumbia macho mtu yeyote atakayebainika kukiuka sheria hizo.

“Katika tukio hilo aliyekuwa anaendesha gari siyo dereva aliyeajiriwa ni utingo kwa hiyo tuko hapa kusimamia usalama wa watu waliokusanyika hapa na kuyasogeza pembeni na kuhakikisha njia inapitika,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kahama mkoani humo, Hafidhi Omari amesema baada ya kupata taarifa ya ajali hiyo, wamefika eneo hilo na kuanza kuzima moto huo ambapo wamefanikiwa ndani ya dakika saba.

“Baada ya kufika eneo la tukio gari zote zilikuwa kwenye zinaungua lakini gari namba T195 EEY ilikuwa inaungua  zaidi na tulianza kupambana na moto huo dakika tano mpaka saba tuliweza kuuzima kabisa,” amesema Omari.

Waliokufa walikuwa wanatuita

Akisimulia tukio hilo lilivyokuwa, shuhuda wa ajali hiyo, Welnton Mngeja amesema baada ya magari hayo kugongana na kuwaka moto mmoja wa watu walioteketea alikuwa amenasa huku akiomba msaada wa kunasuliwa ndani ya gari hilo.

“Hao waliokufa wameteketea mulemule mpaka mmoja alikuwa anatufanyia hivi (kuwaita) sasa tukashindwa moto ulikuwa unazidi kuwa mkubwa hadi tukasambaa,” amesema Mngeja.

Shuhuda mwingine, Denis Temba amesema baada ya lori lililokuwa likitokea uelekeo wa Dar es Salaam kumshinda dereva na kubadili uelekeo liligongana uso kwa uso na lori lingine kisha kuwaka moto.

Related Posts