47 CCM wautaka ubunge wa Afrika Mashariki

Dar es Salaam. Wagombea 47 kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) wamejitokeza kuwania nafasi moja ya ubunge katika Bunge la Afrika Mashariki.

Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa Bunge hilo katika kundi la wanawake kupitia CCM, Dk. Shongo Sedoyeka, kilichotokea Juni 13, 2024.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linatakiwa kufanya uchaguzi mdogo wa mbunge ili kujaza nafasi hiyo kulingana na kanuni.

Mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu uliofanyika kwa siku sita kuanzia Agosti 10 na kuhitimishwa jana Agosti 15 umewaibua wagombea 47 wanaowania nafasi hiyo.

Mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu umefanyika katika Makao Makuu ya CCM Dodoma, Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar, na Ofisi ndogo ya CCM, Dar es Salaam.

Akizungumzia mchakato huo, msimamizi wa Dodoma, Saad Kusilawe, amesema shughuli hiyo imehitimishwa kwa wagombea 22 kujitokeza kuchukua fomu mkoani humo.

“Dar es Salaam waliochukua fomu ni 24 na Zanzibar amejitokeza mmoja pekee,” amesema Kusilawe.

Amesema baada ya uchukuaji na urejeshaji fomu kufungwa, kinachofuata ni vikao vya kuwachambua wagombea wote kisha kufanya uteuzi wa majina yatakayopitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa kabla ya wabunge kuwapigia kura.

Uchaguzi huo utafanyika wakati wa Mkutano wa 16 wa Bunge utakaoanza Agosti 27, 2024.

Related Posts