Klabu ya Simba jana imekamilisha usajili wa Leonel Ateba kutoka USM Alger ya Algeria na saa 4:00 usiku ikamtambulisha rasmi.
Wakati Wanasimba wakitamba na ujio wa Ateba, presha imehamia kwa wachezaji wawili ambao mmojawapo ataonyeshwa mlango wa kutokea ili kumpisha Ateba.
Wachezaji hao ni mshambuliaji Freddy Koublan ‘Fungafunga’ na kipa Ayoub Lakred.
Inaripotiwa kwamba wachezaji hao ndio wamewekwa katika kikaango cha mmoja kuondoka ili kumpisha nyota huyo mpya raia wa Cameroon kwa vile Simba sasa ina wachezaji 13 wa kigeni na kanuni za ligi kuu Tanzania Bara zinalazimisha timu kuwa na wachezaji 12 tu wa kigeni.
Inaripotiwa kwamba hadi sasa, uongozi wa Simba haujaamua nani wa kuwekwa kando kati ya wawili hao na mchana wa leo, Ijumaa, Agosti 17 utatoa uamuzi wa mwisho.
Koublan ameonekana kutomridhisha kocha Fadlu Davids na inaripotiwa kwamba kocha huyo ametoa baraka kwa uongozi kumpiga chini Muivory Coast huyo.
Lakini kwa Ayoub, majeraha yake ya muda mrefu yanawapa wasiwasi Simba kwamba huenda akakosa idadi kubwa ya michezo hivyo naye anafikiriwa kuachwa.
Kinachomuweka Ayoub katika wakati mgumu zaidi ni kipa mpya, Mousa Camara ambaye kiwango alichokionyesha katika mechi tatu alizotumikia timu hiyo, kimewakosha wengi.
Je unadhani nani atapigwa panga na Simba ili kumpisha Ateba?