IKIWA imesalia siku moja tu, kabla ya Yanga kushuka uwanjani kuvaana na Vital’O ya Burundi katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kocha wa kikosi cha wananchi, Miguel Gamondi awachimba biti mastaa wa timu hiyo ili isije ikawakuta aibu mbele ya wapinzani wao hao.
Yanga itakuwa ugenini mbele ya Warundi hao kwente Uwanja wa Azam Complex, kuanzia saa 10:00 jioni ya kesho kabla ya kurudiana wikiendi ya wiki ijayo Kwa Mkapa na mshindi wa pambano hilo atasonga mbele kuvaana na mshindi wa mchezo kati ya SC Villa ya Uganda au CBE ya Ethiopia.
Akizungumza na Mwanaspoti, jana Gamondi alisema, mastaa wa timu hiyo wamekuwa na kiwango bora katika mechi chache walizocheza, ila hawatakiwi kujiamini kuwa watashinda mchezo ujao.
Aidha, alieleza kuwa, aliwaambia hivyo kwani mpinzani wao ni mpya kabisa kwao hivyo wasiwachukulie poa, jambo ambalo halitakiwi katika mpira wa miguu.
“Vital’O ni timu ambayo hatujawahi kucheza nayo hivi karibuni, hivyo wachezaji hawatakiwi kujiamini na matokeo ya mechi zilizopita,” alisema Gamondi na kuongeza;
“Kuwafunga Simba na Azam sio kigezo cha wao kujiamini kupitiliza kuwa na hawa Waburundi watawafunga. Nidhamu ya hali ya juu inatakiwa. Mashindano haya ni tofauti na ligi hivyo huwezi kupima kiwango cha mpinzani, lolote linaweza kutokea.”