KIWANDA KIPYA CHA CHUMVI KUFUNGULIWA LINDI – MWANAHARAKATI MZALENDO

Wizara ya Madini, Wizara ya Mipango na Uwekezaji, na Wizara ya Viwanda na Biashara zimekutana jijini Dodoma mnamo Agosti 15, 2024, kujadili changamoto zinazokabili sekta ya uzalishaji chumvi nchini. Kikao hicho kimeandaliwa kufuatia taarifa zilizowasilishwa kwa Serikali na Chama cha Wazalishaji Chumvi Tanzania (TASPA) kuhusu matatizo yanayoathiri sekta hiyo.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Jaffo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Mh. Prof. Kitila Mkumbo, na Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde walishiriki katika kikao hicho pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya chumvi. Kikao hicho kililenga kutafuta njia za kuimarisha sekta hiyo na kurekebisha matatizo yaliyopo, ikiwemo kudorora kwa biashara ya chumvi nchini.

Katika majadiliano, Wizara ya Madini kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) iliahidi kuhakikisha ufungaji wa kiwanda kipya cha kusindika chumvi katika Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi kabla ya mwisho wa mwezi Desemba 2024. Hatua hii inatarajiwa kuboresha uzalishaji na usindikaji wa chumvi, na hivyo kuondoa changamoto za upungufu wa bidhaa hiyo muhimu.

Wizara hizo pia zilijadili mipango ya kuongeza uwekezaji katika sekta ya chumvi, kuboresha miundombinu, na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, watoa huduma, na wazalishaji wa chumvi. Hatua hizi ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha kuwa sekta ya chumvi inakuwa na tija na inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa taifa.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts